NA MATUKIO DAIMA APP, NJOMBE.
Wamiliki wa maduka ya dawa mhimu za binadamu katika halmashauri ya mji wa Makambako wilayani Njombe wamelalamikia kitendo cha mamlaka zinazohusika na usimamizi wa dawa na vifaa tiba kuondoa na kuzuia baadhi ya dawa zisiuzwe kwenye maduka yao.
Wakizungumza katika semina ya wamiliki na wahudumu wa maduka ya dawa mhimu za binadamu na mamlaka ya dawa na vifaa tiba TMDA kanda ya nyada za juu kusini ambayo imefanyika ukumbi wa KKKT Jogoo Makambako ,wamiliki hao wamesema kitendo cha kuondolewa kwa baadhi ya dawa hasa zile zinazotumiwa na watu wanaoishi na maambukizi ya virusi vya ukimwi ikiwemo septrin inasababisha jamii ipate adha.
Wamiliki hao,Anipe Ngailo,Yusta Mtega na Aloyce Mkungilwa wametaka kurejeshwa kwa mafunzo ya awali ambayo yalikuwa yanatolewa kwa watu wanataka kufanya kazi ya kuuza maduka hayo,huku wakitaka pindi mamlaka inapokamata dawa zisizotakiwa kwenye maduka yao kuzipeleka kwenye vituo vya afya badala ya kuzichoma moto.
Mfamasia wa halmashauri ya mji wa Makambako Neema Mollel amesema changamoto kubwa kwa sasa kwa wahuduma na wamiliki wa maduka ya dawa mhimu za binadamu ni kukosa sifa zinatokiwa ili kufanya kazi hiyo pamoja na kuuza dawa ambazo hazitakiwa kuuzwa.
Naye meneja wa mamlaka ya dawa na vifaa tiba TMDA kanda ya nyanda za juu kusini Anitha Mshigati amewataka wahuduma na wamiliki wa maduka hayo kufuata miongozo ya serikali ikiwa ni pamoja na kutotoa huduma ambazo hawatakiwa kuzitoa ikiwemo kuchoma sindano wagonjwa.
0 Comments