Header Ads Widget

TAKRIBANI HEKTA 470 ZA HIFADHI KANDA KASKAZINI MIKOA YA TANGA KILIMANJARO,ARUSHA NA MANYARA ZIMEATHIRIWA NA MOTO

Na Ashrack Miraji Matukio Daima App 

Takribani Hekta 470 za Hifadhi kanda ya Kaskazini inayojumuisha Mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara zimeathiriwa na moto katika kipindi cha msimu huu wa kiangazi kati ya hizo takribani Hekta 132 zipo Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro ikiwemo baadhi ya maeneo ya Hifadhi ya Msitu Asilia wa Chome (Shengena).

Hayo yamebainishwa na Kaimu Kamanda wa Wakala wa huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Kaskazini Agustine Mathias, wakati wa ufunguizi wa mafunzo ya ufuatiliaji moto katika Hifadhi za Misitu, yanayolenga kuboresha utayari wa Taasisi ya TFS katika kudhibiti matukio ya mioto kwenye Hifadhi za Mazingira Asilia, Hifadhi za Misitu na Misitu ya kupandwa.

Kamanda Agustine Mathias alisema miongoni mwao sababu za kutokea kwa matukio hayo ya mioto ni Imani potofu kwa baadhi ya watu ambao wanashindana kuchoma moto na yule ambaye moto wake utaenda mbali kwamba yeye anaonekana ataishi muda mrefu sana kuliko wenzake. Sambamba na hilo lakini shughuli za kijamii ikiwemo uandaaji wa mashamba, Uvunaji holela wa asali, Uchomaji wa Mkaa na Uwindaji wa Wanyama pori, nazo zinachangia.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Same Kasilda Mgeni ameonya Wananchi kuacha mara moja tabia ya kueneza Imani hizo potofu kwenye jamii, Akisisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kaili kwa yeyote atakaye bainika kuendeleza vitendo hivyo kwani vinapelekea kuwepo kwa uharibifu mkubwa wa Mazingira na kufanya viumbe hai vipotee pia kupoteza kabisa uoto wa Asili kwenye misitu yetu. 

“Haya mafunzo yamekuja wakati muafaka sana, nimekuwa nikitembea kwenye ziara zangu mbalimbali ndani ya Wilaya ya Same kati ya jambo ambalo limenichefua sana ni Wananchi kuchoma moto ovyo jambo ambalo linapelekea kuharibu mazingira yetu ikiwemo maeneo ya Hifadhi zetu”. Alisema DC Kasilda.

DC Kasilda amesisitiza pia pamoja na Wilaya kuchukua hatua za makusudi za kukabiliana na watu wanaoharibu Mazingira kwa kuchoma moto, lakini pia jitihada za pamoja baina ya Serikali ya Wilaya na Taasisi za uhifadhi zinahitajika kuhakikisha wahusika wote wanachukuliwa hatua ili misitu iweze kubaki salama.

Aidha ameelekeza TFS kunapotokea matukio makubwa ya mioto wahakikishe wanashirikiana pia na vyombo vya usalama, ikiwemo chombo chenye dhamana na mambo hayo ambacho ni Jeshi la Zimamoto na uokoaji ili waweze kusaidia kuongeza nguvu kuokoa sehemu ya mazingira dhidi ya majanga hayo.




 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI