Header Ads Widget

SONGWE WAZINDUA KAMPENI MAALUMU YA KUWAREJESHA WATOTO WALIO NJE YA SHULE.

 

                 MKUU WA MKOA WA SONGWE, DANIEL CHONGOLO

Na Moses Ng'wat, Songwe.


SERIKALI Mkoani Songwe kwa kushirikiana na wadau wengine wa elimu imezindua kampeni maalum inayolenga  kuandikisha na kuwarejesha shuleni watoto 11,043 walio nje ya shule.


Hayo yamebainishwa leo Novemba 22, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, wakati akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari.


Chongolo amesema kampeni hiyo ya miaka mitano inakusudia kuondoa vikwazo vya kijamii na kifikra ambavyo vimekuwa vikizuia watoto wengi kuendelea na masomo.


"Hii ni hatua muhimu katika juhudi za kuhakikisha watoto wote wanapata elimu kama haki yao ya msingi, kwani takwimu zinaonesha kuwa idadi ya watoto walio nje ya mfumo wa shule bado ni kubwa mkoani kwetu" .


"Pia kampeni hii inalenga kutatua changamoto za kijamii na kifikra, kuboresha miundombinu ya shule, na kufanikisha lengo la uandikishaji wa asilimia 80% mwaka 2025, kutoka asilimia 44% ya mwaka 2024". Amefafanua zaidi Chongolo.


Amesema kwa kipindi cha miaka miwili, Mkoa hio umeandikisha wanafunzi wa MEMKWA 4,826, wakiwemo wasichana 2,254 na wavulana 2,572. 


Chongolo aliongeza kuwa  wanafunzi 2,037 ambapo wavulana walikuwa 1,172  na wasichana 865 walirejeshwa kwenye mfumo rasmi wa elimu.  


Aidha, Chongolo ametoa wito kwa viongozi wa vijiji kuhakikisha watoto wote walio nje ya shule wanatambuliwa na kurejeshwa shule kama hatua Muhimu za Kufanikisha malengo ya kampeni hiyo.

 

Pia amezitaka kamati za shule kubaini changamoto za watoto na kuweka mikakati ya utatuzi.  


Vile vile amewataka viongozi wa Halmashauri za Wilaya kusimamia uandikishaji wa watoto waliokuwa nje ya shule na kuweka mikakati ya kudhibiti mdondoko wa wanafunzi waliorejea shuleni.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI