Na Moses Ng'wat, Mbozi.
JESHI la Polisi Mkoa wa Songwe limethibitisha kuwashikilia viongozi na wafuasi 12 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiongozwa na Mwenyekiti wao Taifa, Freeman Mbowe, likiwatuhumu kufanya mkutano wa kampeni za uchaguzi wa serikali za Mitaa katika eneo ambalo hawakupangiwa kinyume na ratiba za wasimamizi wa uchaguzi.
Katika kundi hilo la waliokamatwa na kushikiliwa katika kituo cha polisi Vwawa, Wiayani Mbozi, yupo pia Mwenyekiti wa chama cha ACT- Wazalendo Mkoa wa Songwe, Elia Zambi.
Mapema leo Novemba 22, 2024 taarifa zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii zikieleza kuwa Mbowe na wenzake walikamatwa na kupelekwa kwenye mapori, hali ambayo iliibia taharuki kubwa kwa jamii.
Akizunhumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Agostino Senga, alisema viongozi na wafuasi hao walikamatwa katika eneo la Lwati, Wilayani Mbozi baada ya kufurushwa eneo la Mlowo walikokuwa wakilazimisha kufanya mkutano katika eneo kinyume na ratiba ya wasimamizi wa uchaguzi.
Alisema mbali na kosa hilo, viongozi hao wanadaiwa kufanya vurugu wakati wa ukamataji na kujeruhi askari wawili.
Kamanda Senga, aliwataja watu wengine walliokamatwa pamoja na Mbowe kuwa ni Mwenyekiti wa chama hicho, Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu kama sugu, Mbunge Mstaafu wa jimbo la Mbozi, Paschal Haonga na Mdude Nyagali ambaye ni kada maarufu wa chama hicho.
Aliwataja wengine waliokamtwa kuwa ni pamoja na walinzi wa Mbowe, ambao ni Adamu Kasekwa (35), Halfan Mbire (37) na Mohammed Ling'wanya ambapo baada ya kupekuliwa wanadaiwa kukutwa na visu viwili ambavyo ni silaha zisizoruhusiwa kwenye mikutano ya kisiasa.
Kamanda Senga aliwataja watu wengine waliokamtwa kuwa ni maofisa habari (waandishi wa habari) wawili ambao ni Apolinary Margwe kutoka Makao Makuu ya chama, pamoja na ofisa habari kanda ya Nyasa, Keneth Ndabila, huku wengine wakiwa ni ofisa wa kanda ya Nyasa, Paul Joseph na Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Mbozi, Michael Msongole.
Akizungumzia juu ya kiongozi wa ACT- Wazalendo kukamatwa pamoja na viongozi wa Chadema, Kamanda Senga alisema kiongizi huyo ndiye aliyewakaribisha viongozi hao wa chadema kwenda kufanya mkutano wa kampeni katika eneo la Mlowo ambalo hawakupangiwa na wasimamizi wa uchaguzi.
Katika hatua nyingine, Katibu wa Chadema kanda ya Nyasa, Grace Shio, amepinga sababu zilizotolewa na jeshi la polisi juu ya kukamatwa kwa viongozi wao, akieleza kuwa ukamataji uliofanywa sio halali.
Alisema viongozi hao walikamatwa wakiwa wanarejea katika moja ya mkutano wao wa kampeni katika kijiji cha Itewe, kata ya Halungu, Wilayani Mbozi, hivyo hakuna kiongozi aliyefanya mkutano katika eneo ambalo hawakupangiwa.
" Wakati viongozi wetu wanarudi wakiwa katika kijiji cha Halungu walikutana na gari la OCD (Kamanda wa polisi Wilaya) wa Mbozi, lakini wakiwa wanaendelea na safari ghafla mbele walikuta magari, likiwemo la Halmashauri(limetambuliwa) yakiwa yamefunga njia kabla ya askari kuanza kuwashusha viongozi wetu kwenye magari na kuwakamata , akiwemo Mwenyekiti wetu Taifa (Mbowe), Alifafanua Katibu huyo wa kanda ya Nyasa Shio.
Pia alisema kwa mujibu wa ratiba Chama hicho kilikuwa kifanye mikitano yake ya kampeni katika majimbo mawili ya Mkoa wa Songwe ambayo ni Mbozi na Tunduma.
"Wametuharibia mikutano yetu mikubwa ya Vwawa na Tunduma, hivyo tunaomba jeshi la polisi liwaachie viongozi wetu bila masharti.
0 Comments