Na Moses Ng’wat, Tunduma.
WATU Saba wamefariki dunia baada ya Bajaji waliyokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na Lori wakati dereva wa bajaji akijaribu kuyapita magari mengine yaliyokuwa mbele yake katika eneo la Mpemba, Mjini Tunduma, Wilaya ya Momba.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Novemba 23, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga, imeeleza kuwa ajali hiyo ilitokea Novemba 22, 2024 majira ya saa 3:15 usiku.
Alisema kuwa, Bajaji hiyo yenye namba za usajili MC 783 DUF iliyokuwa ikitokea eneo la Mpemba kuelekea Mjini
Tunduma iligongana na Lori aina ya Scania lenye namba T 958 BCS .
Kamanda Senga alisema Bajaji hiyo ilikuwa ikiendeshwa na Emmanuel Hakimu ambaye ni miongoni mwa watu hao saba waliofariki katika ajali hiyo.
Akifafanua Zaidi, Kamanda Senga alisema katika ajali hiyo, watu watano walifariki papo hapo, huku wengine wawili akiwemo mtoto mdogo Isacka Mambwe (2) walifariki wakati wakipatiwa matibabu hospitalini.
Aliwataja waliofariki papo hapo kuwa ni Emmanuel Hakimu,aliyekuwa dereva wa bajaji, wengine ni Rehema Christopher (25), Mkazi wa Msongwa, Festo Mambwe (57), Mkazi wa Mbeya, Rosemary Njema (44), Mkazi wa Ipito Mjini Tunduma na Milembe Siyantemi (36), Mkazi wa Kapele, wilayani Momba.
Kamanda Senga, ameongeza kuwa jeshi hilo linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha ajali hiyo, huku likiendelea kumtafuta dereva wa Lori ambaye alitoweka baada ya ajali hiyo.
"Miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika kituo cha afya Tunduma wilayani Momba na kwamba chanzo cha ajali hiyo bado tunakichunguza, ikiwa ni pamoja na kumsaka dereva wa scania," amesema kamanda Senga.
Pamoja na hayo kamanda Senga amewaasa madereva na wamiliki wa vyombo vya moto kujenga tabia ya kukagua vyombo vyao kabla ya kuanza safari na kuzingatia Sheria za usalama barabarani wakati wote ili kuzuia ajali zinazoepukika.
0 Comments