Header Ads Widget

RC ANDENGENYE ARIDHISHWA WALIOJITOKEZA KUPIGA KURA KIGOMA


Na Fadhili Abdallah,Kigoma

MKUU wa  mkoa Kigoma Thobias Andengenye ameeleza kuridhishwa na idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza kupiga kura kwa ajili ya kuchagua viongozi wa serikali za mitaa katika uchaguzi uliofanyika Novemba 27 mwaka huu.

Akizungumza katika kituo cha Mtendaji wa kata ya Mjini Mtaa wa Shede Manispaa ya Kigoma Ujiji Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa licha ya kuridhishwa na idadi kubwa ya watu waliojitokeza lakini pia upigaji kura umekuwa wa amani na utulivu kutokana na mazingira mazuri yaliyowekwa na serikali ili kuwezesha kila mpiga kura kutimiza wajibu wake wa kidemokrasia.


Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa binafsi ameshawishika kujitokeza kupiga kura kwanza kutimiza wajibu wa kidemokrasia lakini pia kuchagua kiongozi ambaye ndiye mwanzishaji na msimamizi wa mipango ya maendeleo katika mtaa wake hivyo ni muhimu kuchagua kiongozi ambaye ana maono na mwenye uwezo wa kutimiza matakwa ya wananchi katika kuwaletea maendeleo.

Katika hatua nyingine wananchi katika maeneo ya wilaya mbalimbali za mkoa Kigoma wamejitokeza kupiga kura kwa ajili ya kuchagua viongozi wa serikali za mitaa huku wakieleza kuridhishwa na taratibu zilizopo vituoni ambazo zimewezesha kupiga kura kwa amani, usalama bila usumbufu wowote.

 

Mmoja wa wapiga kura hao, Padre Francis Laswai ambaye ni Mkuu wa shule ya sekondari Watakatifu Rufino na Rinaldo kutoka Kijiji cha Kasumo wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma alisema amejitokeza kupiga kura baada ya kuona umuhimu wa kuchagua viongozi watakaowafaa katika kusimamia mipango mbalimbali ya serikali kwa ajili ya maendeleo ya wananchi akieleza kuridhishwa na utaratibu wa kupiga kura uliokuwepo.

Naye Abbas Rashid Mkazi wa Mtaa Mgera B kata ya Mwandiga Halmashauri ya wilaya Kigoma alisema kuwa hadi kufikia mchana hakukuwa na tatizo lolote katika zoezi la upigaji kura tangu kufunguliwa mapema asubuhi ambapo kila mwananchi aliyefika kituoni alihudumiwa na kupata nafasi ya kupiga kura na watu wazima, wajawazito na wagonjwa walihudumiwa mapema na kuondoka.

 

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI