Na Davis Kiwelu
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Philip Isdor Mpango kuwa mgeni rasmi katika Kongamano la Tatu la Kimataifa la Kisayansi la TAFORI litakalofanyika Disemba 11 hadi 13, 2024 katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha, (AICC) mkoani Arusha.
Haya yamezungumzwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), Dk. Revocatus Mushumbusi wakati akizungumza na waandishi wa Habari TAFORI Makao Mkuu, Morogoro, Novemba 15, 2024.
Dk. Mushumbusi amesema kongamano hilo litaongozwa na mada kuu isemayo *“ _Kurejesha Mandhari ya Misitu kwa Maendeleo Endelevu na Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi_”* yaani _Restoring Forest Landscapes for Sustainable Development and Climate Change Mitigation_ ambapo wadau takribani 400 Kutoka ndani na nje ya nchi watapata nafasi ya kujadiliana masuala ya Misitu na Nyuki, ikiambatana na mawasilisho na maonesho ya mazao ya Misitu na Ufugaji Nyuki kutoka kwa wadau.
Wadau hao ni kama vile, wanasayansi, watunga sera, wanamazingira, watumiaji wa mazao ya Misitu na Nyuki, wapanda miti, wafugaji wa Nyuki, Taasisi za utafiti, vyuo vikuu, Taasisi za Kiserikali na zisizo za Kiserikali na wanafunzi.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa TAFORI Dkt. Mushumbusi amesema lengo la kongamano hilo ni;
Moja, kuwakutanisha wataalamu wa Misitu na ufugaji Nyuki, kujadiliana kwa pamoja na kubadilishana uzoefu juu ya usimamizi wa maliasili hasa Misitu na ufugaji Nyuki.
Mbili, Kupitia kongamano hili, wataalamu wa ndani na nje ya nchi wataweza kutumia nafasi hii kutoa matokeo ya tafiti zilizofanyika.
Tatu, kuibua miradi mipya ya uhifadhi kwa lengo la kurejesha na kuongoa Misitu kwa maendeleo endelevu na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Nne, Kuunga mkono jitihada za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizozifanya za kutangaza vivutio vya utalii kupitia filamu ya ‘‘Tanzania The Royal Tour na Amazing Tanzania”.
Vilevile, Kongamano hili litakuwa ni sehemu ya kuchochea na kuhamasisha wadau mbalimbali kushirikiana na Serikali kwenye maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Wafugaji Nyuki Duniani (APIMONDIA) utakaofanyika nchini mwaka 2027.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa TAFORI Dk. Mushumbusi amewasihi wadau kushiriki katika Kongamano hilo kwani kushiriki kwao ni sehemu ya majukumu ya Taasisi katika kuhakikisha inasambaza matokeo ya tafiti za Misitu na ufugaji Nyuki kwa watumiaji wa mwisho nchini Tanzania na kutoa majibu ya changamoto zinazoikabili sekta hiyo.
0 Comments