Na Editha Karlo,App matukio daima Kigoma
MAHAKAMA ya Mwanzo Wilaya ya Kigoma Ujiji imemhukumu Emmanuel Hiraly (19) kifungo cha miezi sita jela kwa kosa la kuiba mita za maji.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Ujiji, Hassan Nuru Galiatano, baada ya mtuhumiwa kukiri kutenda kosa hilo.
Kwa mujibu wa maelezo ya mahakama, Hiraly alitenda kosa hilo Oktoba 21, 2024, katika nyumba ya Juma Rashidi Mpuma, mkazi wa Mtaa wa Kisangani. Alidaiwa kuiba mita na kuziuza kwa bei ya shilingi elfu nne (4,000) kwa kila moja kwa wauzaji wa vyuma chakavu. Hakimu Galiatano alieleza kuwa kitendo hicho ni kinyume na kifungu namba 265 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, toleo la mwaka 2022.
Ingawa Hiraly alikiri kosa na kuomba msamaha, Mahakama iliamua kutoa adhabu hiyo ya miezi sita jela ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo.
Kwa upande mwingine, mshatakiwa wa pili katika kesi hiyo, Said Jaffari (21), alikana kuhusika na wizi huo. Hivyo, kesi yake imeahirishwa na itasikilizwa tena tarehe 21 Novemba, 2024, ambapo pia hukumu yake itatolewa.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Sheria cha Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kigoma (KUWASA), Naaman Kohoye, amepongeza hatua hiyo ya kisheria na kusema kuwa Mamlaka inaendelea kufuatilia na kufikisha mashauri mengine mahakamani yanayohusiana na wizi wa mita na maji.
Kohoye aliwataka wananchi kushirikiana na Mamlaka kwa kutoa taarifa kuhusu wale wanaoharibu au kuingilia miundombinu ya maji ili kuboresha huduma ya majisafi kwa jamii. Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Mamlaka na wananchi ni muhimu kwa kudhibiti uharibifu na kuhakikisha huduma endelevu.
0 Comments