Mkuu wa Wilaya ya Monduli Festo Kiswaga ameagiza jamii kuzingatia umuhimu lishe Bora kwa watoto ili kuepukana na udumavu.
Kiswaga ametoa Rai hiyo leo katika wakati wa maadhimisho ya Lishe ngazi ya wilaya yaliyofanyika kata ya Migungani katika Halmashauri ya Monduli .
Alisema kuwa Suala la lishe Bora ni muhimu kwa jamii kuendelea kuzingatia kwani ili kuwa na Familia Bora na Taifa Bora ni lazima lishe ipewe kipaumbele kwa watoto kwa kuwa watoto wenye lishe bora hata Uwezo Wao wa kiakili huwa mkubwa na mwisho wa Siku ndio Taifa bora.
Alisema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa Mbele kuhamasisha lishe Bora na ni vema Kila mmoja kuweka mkazo wa lishe bora kwa watoto .
Pia Kiswaga aliwataka wanawake wenye watoto wanaonyonya kuzingatia unyonyeshaji mzuri wa watoto kwa kwani kunyonyesha maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo pamoja na matumizi ya vidonge vya kuongeza damu kwa wajawazito iwe kipaumbele .
Alisema kuwa lengo la maadhimisho haya ni kutoa elimu kuhusu lishe bora na kuhamasisha jamii ili kuepuka magonjwa yanayotokana na lishe duni kama vile kisukari, shinikizo la damu, utapiamlo, na upungufu wa damu kwa wajawazito na watoto wachanga.
Ifahamike kuwa maadhimisho ya Siku ya Lishe kufanyika kila robo mwaka katika ngazi ya kijiji .
Hivyo aliitaka jamii kuchangia chakula kwa watoto mashuleni, kuanzisha klabu za lishe mashuleni, na kutumia vyakula vilivyorutubishwa kwa madini na vitamini muhimu.
"Lishe bora ni moja ya haki za msingi za binadamu, inayopaswa kuheshimiwa, kulindwa, na kutekelezwa kikamilifu"
Alisema kuwa wilaya ya Monduli inaendelea kutekeleza afua mbalimbali za lishe kwa kushirikiana na watendaji wa kata, vijiji, wenyeviti wa vitongoji, wahudumu wa afya ngazi ya jamii, na wadau mbalimbali.
Lengo likiwa ni kuboresha afya na lishe ya watoto, vijana balehe, wajawazito, wanaonyonyesha, wazee, na jamii kwa ujumla.
Mganga mkuu wa Wilaya, Dkt. George Kasbante, alisema kuwa lishe bora ni muhimu kwa wakazi wa Kata ya Migungani na Wilaya nzima kwa ujumla.
Kwani alisema kuwa suala la lishe bora liwe agenda ya kudumu katika vikao vya vijiji, kata, na ngazi ya tarafa.
Kitindi Sayore Afisa Muuguzi wa Kitengo cha Mama na Mtoto katika Hospitali ya Wilaya ya Monduli, alisema kuwa umuhimu wa lishe kwa mama mjamzito na mama anayenyonyesha.
Alisema ili mama mjamzito aweze kujifungua mtoto mwenye afya bora kimwili na kiakili, ni muhimu apate lishe bora katika kipindi chote cha ujauzito, hasa katika siku elfu moja (1000) za mwanzo za maisha ya mtoto, ambazo ni msingi wa ukuaji na maendeleo yake.
Huku afisa Lishe wa Wilaya, Michael Mhombo alizitaja changamoto kubwa kuwa ni tabia ya baadhi ya wananchi kula vyakula ambavyo si mchanganyiko na vina upungufu wa virutubishi.
Kama virutubishi vinavyopatikana kwenye matunda, mbogamboga, na mazao ya wanyama kuwa tabia hiyo husababisha hatari ya utapiamlo na magonjwa sugu yasiyoambukiza, na kupelekea ongezeko la wajawazito wenye upungufu wa damu.
Hata hivyo Wananchi walioshiriki katika maadhimisho haya walitoa shukrani zao kwa uongozi wa wilaya kwa kuwawezesha kupima hali zao za afya na kujifunza kuhusu faida za ulaji wa vyakula mchanganyiko.
0 Comments