Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
JESHI la Polisi nchini Tanzania limesema linawafuatilia kwa karibu baadhi ya watu wanaohamasisha kujiingiza kwenye vitendo vya kihalifu pamoja na matamshi na jumbe zinazotengenezwa na baadhi yao na kuzisambaza mtandaoni kwa lengo la kuleta taharuki kwa jamii.
Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania Naibu Kamishna wa Polisi DCP David Misime ameviambia vyombo vya habari leo Jumapili Februari 22, 2026 kuwa ufuatiliaji huo unafanyika usiku na mchana, akiwataka wananchi kutokuwa na hofu na kuendelea na shughuli zao za kiuchumi na kijamii kama kawaida.
Polisi pia imetoa wito kwa wananchi kuendelea kuwapuuza watu hao na wengineo pamoja na taarifa na jumbe zao kwani watu hao hawapo ndani ya mipaka ya nchi na hata wanachokihamasisha hawatashiriki na hawatokuwa na uwezo wala mwanya wa kushiriki.
"Wananchi watambue lengo la watu hao ni kutaka kutuchonganisha, kutujengea chuki ili tuhamasike kujiingiza kwenye uhalifu na vitendo vya vurugu. Jeshi la polisi halitasita kumchukulia hatua yeyote yule atakayeendelea kujihusisha na vitendo kama hivyo au kujiingiza katika uhalifu wa aina yoyote ile kwani ni kinyume cha sheria." Amesema Kamanda Misime.
Polisi imewataja baadhi ya watu wanaoshawishi uhalifu kuwa ni pamoja na anayejitambulisha kwa jina la TFF ambaye amekuwa akitoa taarifa mbalimbali ikiwemo kufanya mazoezi porini na kwamba wameshafanya matukio kadhaa ya kijinai ambapo Polisi imekanusha taarifa hizo zote zinazotolewa na mtu huyo kwenye mitandao.






0 Comments