Header Ads Widget

WAZIRI DKT CHANA KUHITIMISHA KILELE CHA MAADHIMISHO YA MIAKA 60 YA HIFADHI YA RUAHA KESHO

 

NA MATUKIO DAIMA MEDIA 

WAZIRI  wa Maliasili na utalii Dr Pindi Chana anatarajiwa  Mgeni rasmi katika kuhitimisha Kilele Cha  maadhimidho ya Miaka 60 ya kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha mkoani Iringa kesho jumatatu.

Maadhimisho hayo yaliyoanza Octoba 1-7 mwaka huu kwa kufanyika shughuli mbali mbali za kuhamasisha utalii na utoaji elimu ya utalii  yatafanyika ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

 Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Godwell Ole Meing'ataki,akiwa katika kipindi Cha Tanzania ya Leo kilichorushwa na Runinga ya mtandaoni ya Matukio Daima Tv ameeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya hifadhi hiyo katika kipindi cha miaka 60 ya kuanzishwa kwake.

 Kuwa serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 60, kiasi ambacho kimechangia kupanda kwa idadi ya wageni wanaotembelea hifadhi hiyo.

Alisema kuwa serikali imeboresha miundombinu kwa kujenga nyumba za wageni, watumishi, madereva na sehemu za kupumzika, hali ambayo imeongeza urahisi kwa wageni na kuchangia ukuaji wa sekta ya utalii. 

"Hapo awali, kulikuwa na uhaba wa miundombinu ya kuhudumia wageni, lakini sasa nyumba za watumishi na madereva zimeboreshwa, pamoja na ujenzi wa vyumba vya familia na hosteli mpya yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi zaidi ya 40," alisema.

Meing'ataki pia aliongeza kuwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amechangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza utalii wa ndani kupitia filamu ya "The Royal Tour," ambayo imewawezesha Watanzania, hususan wanawake, kuona umuhimu wa kutembelea hifadhi za taifa. 

"Filamu hiyo imeibua hamasa kubwa kwa Watanzania, jambo ambalo limechangia ongezeko la idadi ya watalii wa ndani," alieleza.

Akielezea upekee wa Hifadhi ya Ruaha, Meing'ataki alisema hifadhi hiyo inajivunia kuwa na idadi kubwa ya tembo, simba, na nyati, ambao ni vivutio vikubwa kwa watalii. Hifadhi hiyo pia ina eneo kubwa, ambapo asilimia 30 pekee ya hifadhi hutumika kwa shughuli za utalii.

Aidha, alieleza mafanikio ya ujirani mwema kati ya hifadhi na jamii inayozunguka, akisema kuwa uhusiano mzuri umepelekea kupungua kwa ujangili na uharibifu wa mazingira. 

Wananchi wamekuwa wakishirikishwa katika uhifadhi, wakipewa elimu na kuhamasishwa kushiriki kwenye miradi ya maendeleo.

Meing'ataki alihitimisha kwa kusema kuwa Hifadhi ya Ruaha pia imekuwa msaada mkubwa kwa jamii jirani kwa kutoa ufadhili wa masomo, ujenzi wa shule, na kusaidia miradi ya wanawake kwa mikopo yenye riba nafuu. 

Kuwa haya yote yamekuwa chachu ya maendeleo katika sekta ya utalii na uchumi wa taifa.


Alisema kuwa Hifadhi imefanya  imarisha uhusiano na jamii mbalimbali, ikiwemo watu wenye ulemavu,wazee wa kimila na viongozi wa dini  kwa lengo la kuwapatia fursa ya kutembelea hifadhi hiyo pamoja na kutoa msaada kwa familia zenye mazingira magumu

“Nitumie fursa hii kuwakaribisha Watanzania wote, hususan wakazi wa Iringa, katika maadhimisho ya miaka 60 ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambayo yatafanyika yaliyoanza  tarehe 1 hadi 7 Oktoba, 2024 Siku ya  kilele chake Cha maadhimisho hayo"

Alisema kuwa  mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho hayo Balozi Dkt. Chama  ambaye atahitimisha shughuli hiyo kwa kuzindua rasmi utalii wa puto. 

Kuwa huduma hii mpya ya utalii wa puto inalenga kuwavutia watalii zaidi katika hifadhi hiyo kwa kuwapa fursa ya kufurahia mandhari ya kuvutia ya Ruaha kutoka angani.


Meing’ataki alieleza kuwa ziara maalum kwa Chifu wa kabila la Wahehe na viongozi wake wa kimila, pamoja na viongozi wa dini na makundi mengine zimekuwa na hamasa kubwa ya kuhamasisha utalii wa ndani .


Pia, alisema kupitia  kongamano maalum la miaka 60 ambalo lilijikita katika kujadili historia ya hifadhi hiyo, mafanikio yaliyopatikana na changamoto zilizopo, sambamba na kutoa mapendekezo ya namna ya kuimarisha uhifadhi wadau wamepata Mwanga Bora wa Hifadhi hiyo.

Alisema Hifadhi ya Taifa ya Ruaha imepiga hatua kubwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 1964. 

Alisema awali, hifadhi hiyo ilikuwa na ukubwa wa kilomita za mraba 9,500, lakini sasa imeongezeka na kufikia kilomita za mraba 19,822.

 Kuwa Ongezeko hili limechangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa mkoa wa Iringa na taifa kwa ujumla hivyo  Ruaha inajivunia kuwa na idadi kubwa ya wanyama wa aina mbalimbali. 

Kwa sasa, hifadhi hiyo inakadiriwa kuwa na tembo wapatao 15,000, nyati 20,000, simba zaidi ya 8,000, pamoja na wanyama wengine na ndege wa aina mbalimbali.

Hali hii imeifanya Ruaha kuwa moja ya vivutio muhimu kwa watalii wa ndani na nje ya nchi.

Meing’ataki aliongeza kuwa maboresho makubwa yamefanyika katika miundombinu ya hifadhi hiyo, ikiwemo maeneo ya mapokezi, malazi, na barabara, jambo ambalo limeongeza ufanisi katika kutoa huduma bora kwa wageni wanaotembelea hifadhi hiyo.

Mbali na kuwa kivutio kikubwa cha watalii, Hifadhi ya Taifa ya Ruaha pia ina mchango mkubwa katika uchumi wa taifa. 

Mto wa Ruaha, ambao unapita ndani ya hifadhi hiyo, ni chanzo muhimu cha maji kwa bwawa la Mtera, ambalo linachangia kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa umeme nchini.

 Hivyo uhifadhi wa mto huo unasaidia kuhakikisha uzalishaji endelevu wa nishati ya umeme ambayo inategemewa na taifa.

Hifadhi ya Ruaha pia inachangia kwa kiasi kikubwa mapato ya kigeni kupitia utalii.

Kuwa  watalii wanaotembelea hifadhi hiyo hulipa ada mbalimbali za kuingia, malazi, na huduma nyinginezo, ambazo huingiza mapato makubwa kwa taifa.

Alisema katika kuelekea maadhimisho haya, Meing’ataki alitoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki maadhimisho hayo .

 Kuwa ni muhimu Watanzania, hususan watoto, wawe na utamaduni wa kupenda na kuthamini vivutio vya ndani ili kuunda kizazi chenye mwamko wa uhifadhi wa maliasili na urithi wa taifa kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI