Na Matukio Daima media
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Apimondia Kamisheni ya Afrika, Bw. David Mukomana kwa lengo la kutoa taarifa ya hali iliyofikiwa katika maandalizi ya mkutano wa 50 wa Dunia wa Ufugaji Nyuki (APIMONDIA) utakaofanyika mwaka 2027 nchini Tanzania.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika leo Oktoba 30,2024 jijini Dodoma, Mhe. Chana amemuhakikishia Bw. Mukomana utayari wa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha uwepo wa ukumbi utakaotosheleza washiriki wa mkutano huo.
Kwa upande wake, Bw. Mukomana ameipongeza Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa mkutano huku akisisitiza kuwa hiyo ni hatua muhimu ya kukuza sekta ya ufugaji nyuki na uhifadhi nchini.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano huo nchini, Prof. Dos Santos Silayo alitoa taarifa ya maandalizi yaliyofikiwa ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa kamati jumuishi ya maandalizi, kamati mbalimbali za usimamizi wa masuala ya udhamini, itifaki n.k.
0 Comments