NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu za kuomba kugombea nafasi linatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 22, 2024 baada ya kuanza jumatatu hii (Oktoba 21, 2024) ambapo katika mamlaka ya mji mdogo wa Mbalizi baadhi ya watia nia wa Chama cha Mapinduzi wamesema watahakikisha wanashinda kuendelea kuongoza mamlaka hiyo.
Kada wa Chama hicho (CCM) wilayani Mbeya vijijini (kichama) Lameck Nyirenda ambaye pia aliwahi kutia nia ya udiwani kata ya Utengule Usongwe na Uenezi wa CCM Wilaya ya Mbeya vijijini, amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chama hicho ili kugombea uwenyekiti wa kitongoji akisema anao uwezo kutokana na utumishi wake ndani ya CCM hadi ngazi za wilaya na mkoani.
"Mimi ninatosha kuwa mwenyekiti wa kitongoji cha Utengule hivyo endapo nitateuliwa na Chama chetu (CCM) nitashirikiana na wenzangu kuhakikisha tunaleta mabadiliko ya kimaendeleo, mwenyekiti aliyepo madarakani (bila kumtaja jina) yako mengi amefanya lakini kuna mapungufu kwahiyo moja ya vipaumbele vyangu ni kusoma mapato na matumizi hili limekuwa tatizo kwa wananchi wengi", amesema Nyirenda.
Pamoja na kada huyo wa CCM kugombea kitongojini pia mwanachama John Nzowa, amejitosa pia kuomba kuteuliwa na CCM kugombea nafasi hiyo ili kuhakikisha anakiletea ushindi chama chake na kuwaletea maendeleo wananchi na kwamba wapinzani hawatafanikiwa kwakuwa CCM ndiyo yenye ilani inayotekelezeka.
Jumanne hii (Oktoba 22, 2024) itakuwa ni zoezi la urejeshaji fomu za kuomba kugombea nafasi mbalimbali ndani ya Chama Cha Mapinduzi kisha hatua nyingine za michujo kisha Oktoba 26, kupata wapeperusha bendera watakaopambana na vyama vya upinzani.
0 Comments