Header Ads Widget

MAKALA:SERIKALI KUSOMESHA WATAALAMU BINGWA BOBEZI WASIOPUNGUA 300

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima App, Dodoma

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kufanya mageuzi makubwa ndani ya Sekta ya Afya, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za matibabu, hasa ya kibingwa na ubingwa bobezi hapa nchini.

Katika kufanikisha azma ya kuwa na wataalamu wenye ujuzi wa kutosha wa kutoa huduma bora za matibabu hapa nchini, Wizara ya Afya ilijiwekea lengo la miaka mitano (2020-2025). Waziri wa Afya Jenista Mhagama amesema Wizara ya Afya ilijiwekea lengo hilo la kusomesha wataalamu bingwa na wabobezi wasiopungua 300 kwa kila mwaka wa fedha kupitia Mpango wa Ufadhili wa Masomo wa Serikali unaojulikana kama ‘Samia Health Specialization Scholarship Program’.

Amesema jitihada hizo zimelenga kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya, kupunguza rufaa za matibabu nje ya nchi na hivyo kupunguza gharama kwa Serikali na wananchi pamoja na kuvutia tiba utalii.

"Kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali kupitia Wizara ya Afya imetenga jumla ya Shilingi Bilioni 14, ikiwa ni ongezeko la shilingi Bilioni 3.05 sawa na asilimia 28 zaidi ya bajeti iliyotengwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ya Shilingi Bilioni 10.95," amesema Waziri Mhagama.

"Fedha hizi zilizotengwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025 zitatumika kugharamia mafunzo kwa wataalamu wapya 544 kwa mafunzo ya Ubingwa na Ubingwa bobezi pamoja na wataalamu wengine 47 kwa utaratibu wa seti," ameongeza Waziri Mhagama.

Aidha, amesema wataalamu 829 wanaoendelea na masomo ya ubingwa na ubobezi katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi wataendelea kupewa ufadhili kupitia fedha hizo.

"Kwa mwaka huu wa fedha 2024/2025, Wizara ilipokea jumla ya maombi ya ufadhili 948 nchi nzima, kati ya hao waombaji wa jinsia ya kike ni 353 sawa na asilimia 37 na ya kiume ni 595 sawa na asilimia 63. Kati ya hao, waombaji 771 walikidhi vigezo vya kufadhiliwa na waliochaguliwa kwa ajili ya ufadhili ni 544 sawa na asilimia 71 ya waombaji waliokidhi vigezo," amesema.

Na kuongeza, "Kati ya watumishi 544 waliochaguliwa kupata ufadhili, jinsia ya kiume ni 338 (62%) na jinsia ya kike ni 206 (38%). Watumishi waliochaguliwa kupata ufadhili katika vyuo vya ndani ya nchi ni 517 (95%) na nje ya nchi 27 (5%)," amesema.

Ameeleza kuwa kwa takwimu hizo, kumekuwa na ongezeko la kufadhili watumishi wanaoomba kusomeshwa na Serikali kutoka asilimia 56 mwaka 2022/2023 hadi asilimia 71 mwaka 2024/2025.

Sambamba na hilo, amesema Serikali ya awamu ya sita kwa kuona umuhimu wa uwekezaji katika Sekta ya Afya imeshatumia jumla ya Shilingi Bilioni 30.95 katika kuendeleza wataalamu bingwa na bobezi katika sekta ya afya nchini.

Hata hivyo, Wizara imezingatia vipaumbele muhimu vya kisekta kama ubobezi (super-specialization) katika ngazi mbalimbali za huduma pamoja na vipaumbele kama vilivyoainishwa kwenye Mpango Mkakati wa tano wa Sekta ya Afya (Health Sector Strategic Plan V-HSSP V) pamoja na bajeti ya Wizara ya mwaka 2024/25.

Taaluma hizo ni pamoja na taaluma za watoto wachanga (Neonatology), afya ya akili (Mental health), magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) kama magonjwa ya moyo (Cardiology), matibabu ya ubongo na mishipa ya fahamu (Neurosurgery), huduma za utengamao na tiba shufaa (rehabilitation and palliative services), ugunduzi wa magonjwa ikiwemo patholojia, ni mifano ya vipaumbele vyetu.

Pia amesema kipaumbele kimetolewa kwa watumishi wanaofanya kazi kwenye maeneo yenye uhaba mkubwa wa wataalamu bingwa kwa kuzingatia uwiano wa kijiografia.

"Hivyo watumishi wote waliopata ufadhili kwa mwaka 2024/2025 wanapaswa kukamilisha taratibu," na kuongeza "pia wajeze mikataba ya ufadhili kama kigezo cha kukubali ufadhili huu kabla ya tarehe 01 Novemba, 2024. Nakala ya mikataba hiyo inapatikana kwenye tovuti ya Wizara na pia itatumwa kwa barua pepe kwenye anuani walizotumia wakati wa kuwasilisha maombi."

Amesema ufadhili huu ni kwa ajili ya kulipiwa ada ya mafunzo na posho ya utafiti kwa watakaofadhiliwa ndani ya nchi. Aidha, kwa wale wanaosoma vyuo vya nje ya nchi watalipiwa ada, posho ya kujikimu wakiwa masomoni (Stipend), nauli ya kwenda na kurudi pamoja na posho ya utafiti.

Malipo ya posho ya utafiti na posho ya kujikimu yatazingatia viwango vilivyopangwa na Wizara.

"Nichukue fursa hii kuendelea kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza kwenye Sekta ya Afya hususani katika kuendeleza wataalamu bingwa na bobezi ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata matibabu ya kibingwa na kibobezi yanayotolewa na wataalamu wetu wa ndani," amesema.

Amesema uwekezaji huu ni wa kimkakati utakaoleta tija kwa miaka mingi ijayo kwa kuongeza wigo wa wataalamu bingwa na bingwa bobezi watakaotoa huduma bora kwa wananchi.

"Hii ni dhamira ya dhati ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuishi Mpango Mkakati wa Tano wa Sekta ya Afya kwa kutomwacha mtu yeyote nyuma (Leave no one Behind) katika kuleta maendeleo ya sekta ya afya na nchi kwa ujumla," amesema.

"Nichukue fursa hii kuwashukuru wafanyakazi wa Wizara na Sekta ya Afya kwa ujumla kwa kazi kubwa wanayoifanya kuwahudumia wananchi katika ngazi zote za kutolea huduma. Niendelee kuwatia moyo kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuboresha mazingira ya kufanyia kazi," amesema.

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Molell, hivi karibuni alisema Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imetenga fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za afya, ikiwa ni pamoja na kusomesha wataalamu ndani na nje ya nchi ili wananchi wengi waweze kupata matibabu ya kibingwa ya magonjwa mbalimbali yakiwemo ya moyo.

Naibu Waziri huyo alisema huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo zinazotolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa hospitali hiyo.

Dkt. Molell alimshukuru  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha huduma za afya na hivyo kuwafanya Watanzania na ambao siyo Watanzania kuwa na uhakika wa kupata matibabu ya kibingwa na ndiyo maana Tanzania inapokea wagonjwa kutoka nchi za jirani ambao wanakuja kutibiwa hapa nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mafunzo Wizara ya Afya, Dkt. Saitore Laizer, amesema mpaka sasa kuna wataalamu 805 ambapo uhitaji ni 1486, hivyo serikali kusomesha wabobezi itakwenda kusaidia zaidi.

"Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan sasa inakwenda kusomesha wataalamu hao wa kibingwa na wakibobezi wasiopungua 300. Hatua hii inakwenda kusaidia kupunguza uhitaji kwenye maeneo yenye upungufu wa madaktari bingwa na bobezi katika sekta ya afya," amesema.

Wananchi na wakazi wa Dodoma wameonesha kufurahishwa na jitihada hizo za serikali za kuhakikisha wananchi wake wanapata matibabu yenye ubora hapa nchini.

Sudi Daudi, Mkazi wa Uhindini Dodoma, akiongea na Matukio Daima, kwa niaba ya wananchi wenzake, ameishukuru serikali kwa jitihada hizo na kusema hatua hiyo itapunguza safari za nje ya nchi kwenda kufuata huduma za kibingwa na bobezi.

"Tumekuwa tukisikia serikali inatumia fedha nyingi kufadhili wagonjwa hivyo kwa hatua hii itasaidia kuepuka gharama hizo, " Amesema

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI