Header Ads Widget

WASIMAMIZI WA MIKOPO YA ASILIMIA 10 NGAZI YA KATA WAPATIWA MAFUNZO

  

Na Mariam Kagenda Kagera 

Wasimamizi wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya Wanawake ,Vijana na watu wenye Ulemavu ngazi ya kata ambao ni Maafisa watendaji wa kata na Maafisa maendeleo ya Jamiii katika Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera  wameanza kupatiwa mafunzo ambayo yanalenga kuwawezesha  kupata ujuzi, kuboresha utendaji kazi na kuimarisha usimamizi wa mikopo ya Vikundi vya Vijana , Wanawake na watu wenye Ulemavu .


Wakati akifungua Rasmi Mafunzo hayo  Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba Bwana Jacob Nkwera  amesema kuwa mafunzo hayo yatafanyika kwa siku tano ambapo watendaji wa kata watapata mafunzo hayo kwa siku 2 na maafisa maendeleo ya Jamii wa kata siku 3.

Bwana Nkwera amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwani yatawasaidia wasimamizi hao kutekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuendeleza shughuli za vikundi vya Vijana,Wanawake na watu wenye Ulemavu hivyo ana imani kuwa  watakuwa tayari kutekeleza jukumu hilo muhimu mara baada ya kupata mafunzo hayo 

ameongeza kuwa Mikopo kwa Vikundi hivyo itatolewa kwa mujibu wa sheria ya  fedha ya Serikali za mitaa  Sura namba 290 kifungu cha 37A  ambapo  kifungu hicho kimefafanua kuwa mamlaka za serikali za mitaa zitakuwa na wajibu wa kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani yasiyolindwa  ya mwaka husika kwa ajili ya vikundi hivyo ikiwa ni  sehemu ya fedha zinazotengea kwa ajili ya Shughuli za  maendeleo .


Kwa kuzingatia kifungu hicho halmashauri ya  Manispaa ya Bukoba  imetoa  kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 627 kwa ajili ya mikopo hiyo.ikumbukwe kuwa utoaji wa mikopo ya Vikundi vya Vijana, Wanawake na watu wenye ulemavu ilisitishwa  April mwaka  2023 ili kufanya maboresho ambayo yanaweza kuweka urahisi wa utoaji wa mikopo hiyo na kwa sasa tayari Serikali imeboresha kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo hiyo ili kuleta ufanisi na tija katika utoaji wa mikopo na hivyo kutimiza hadhima ya Serikali ya kuwawezesha wananchi kiuchumi na kupunguza hali ya umaskini  

Kwa upande wake mkuu wa idara ya  maendeleo ya Jamii Manispaa ya Bukoba Bi Hellen Rocky amesema kuwa kwa sasa wasimamizi wa mikopo ngazi ya kata watakuwa ni watendaji wa kata ambao ni wenyeviti  wa kamati za mikopo na maafisa maendeleo ya jamii ya kata watakuwa ni makatibu wa kamati ya mikopo ya kat  .

Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru serikali kwa kuweka utaratibu mzuri wa vikundi hivyo kupata mikopo ya asilimia 10 hasa ikiwa ni pamoja na kuweka wataalamu katika utaratibu wa utoaji wa mikopo hiyo.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI