Na Matukio Daima Media, Simiyu.
CHAMA Cha Wanunuzi wa Pamba nchini (TCA), kimesema zaidi ya kilo Mil. 143 za pamba zimenunuliwa katika msimu wa mwaka huu, tofauti na mwaka jana ambazo walinunua kilo Mil. 270 kufikia wiki ya 23.
Imeelezwa kuwa takwimu hizo zinaashiria kushuka kwa uzalishaji kutokana na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa ikiwemo mvua kubwa na ukame kwenye baadhi ya maeneo ya uzalishaji.
Hayo yamebainishwa na Katibu wa TCA, Boaz Ogolla wakati akiongea na waandishi wa Habari ambapo alisema licha kupunguza uzalishaji lakini wakulima wamenufaika kwa kuuza kwa bei ya juu.
"Soko la kimataifa limeendelea kuporomoka hadi Senti 67, wakati tunafanya hesabu ya mkokotoo ilikuwa Senti 72 ikapanda hadi Senti 75 na ikashuka...kipindi imeshuka, bei ya mkulima iliendelea kupanda ambapo Wanunuzi wameambulia hasara lakini mkulima amepata motisha na watalima zaidi" amesema Ogolla.
Katibu huyo ameeleza kuwa ubora wa Pamba umeshuka kutoka na Pamba kununuliwa kwa soko huria ambapo Pamba imevunwa na takataka katika maeneo ya Meatu, Kishapu na Igunga.
Ameitaka serikali kupitia Bodi ya Pamba kuendelea kutoa Elimu ili wakulima wavune Pamba safi yenye ubora na kukidhi soko la Kimataifa pamoja na kuzingatia utunzaji.
Afisa Kilimo kutoka Kampuni ya alliance Ginnery, Marieta Maduka amesema wanafanya kazi kwa kushirikiana na Maafisa kilimo wa serikali Kwa lengo la kuwahudumia wakulima wa Pamba.
Anasema wamejipanga ili kuweza kuwafikia wakulima moja kwa moja katika mashamba yao vijijini kupitia wakulima viongozi ili kutoa mafunzo ya kuongeza tija ya zao la Pamba.
Ameongeza kuwa wanatumia mbolea zisizokuwa na gharama kwa mkulima kwenye Kilimo hai na kwamba unaandaji wake hauna madhara na kwamba mbolea chai inaongeza uzalishaji na mavuno kwa mkulima.
0 Comments