Na Heriet Molla
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), limesema kuwa limeridhishwa na Mradi wa Utafiti wa Mafuta ghafi na gesi kwenye Bonde la Eyasi Wembere lililopo katika mikoa ya Simiyu, Singida na Arusha.
Utekelezaji wa Mradi huo umefikia asilima 40, ambapo Mradi huo unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi Bil. 40 na Utafiti huo ulianza mwaka 2015.
Akitoa taarifa mbele ya Wajumbe wa Bodi ya TPDC waliotembelea mradi huo mwishoni mwa wiki Jana, Kaimu Meneja wa Utafutaji kutoka TPDC, Saimon Nyalusi amesema shughuli zinazafanyika ni uchukuaji wa taarifa (Data) kwa njia ya mitetemo na kuzichakata ili kuwa na uhakikia wa uwepo wa mafuta au gesi.
Amesema kuwa utafiti unaendelea kufanyika katika bonde hilo kwenye maeneo mawili ya nchi kavu na eneo la ndani ya Ziwa Eyasi.
Ameongeza kuwa katika eneo la Nchi kavu, wamefanikiwa kufikia asilimia 40 ya utafiti na kwamba pameanza kuonekana kwa viashiria mbalimbali ambavyo vimetoa matumaini makubwa ya uwepo wa mafuta na gesi.
“ Utafiti huu ulianza toka mwaka 2015, tumepitia hatua mbalimbali, ambapo kwa hatua hii ambayo tunaendelea kutekeleza, tumeanza kuona mafanikio makubwa, tuko asilimia 40 ya utafiti wetu na tumeanza kuona viashiria vikubwa vya uwepo wa mafuta,” amesema Nyalusi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji kutoka TPDC, Derick Moshi amesema kuwa utafiti huo ni moja kati ya miradi ya kimkakati ambayo serikali inatekeleza kupitia TPDC.
Amesema kuwa kutokana na majibu ambayo yameanza kuonekana, kuna uwezekano wa nchi yetu hadi kufikia mwaka 2026 na 2027 kuanza kuchimba mafuta kwa mara ya kwanza katika historia yake.
“ Kwa jinsi mambo ambavyo yanaonekana kwenda, na taarifa za awali ambazo zimepatikana katika utafiti huu, kuna uwezekano mkubwa kwa mara ya kwanza nchi yetu kuanza kuchimba mafuta kati ya mwaka 2026 au 2027,” amesema Moshi.
Akizungumza kwa niaba Bodi, mjumbe wa Bodi Balozi Peter Kallaghe amesema kuwa wameridhishwa na shughuli zinazoendelea kutekelezwa katika mradi huo huku akiwasisitiza kuongeza kasi ya Utafiti.
“Kwa niaba ya wajumbe wa Bodi, kama wasimamizi wa TPDC, tumejionea mradi na tumeridhika na kazi zinazoendelea kufanyika, ambacho tumesisitiza ni mkandarasi aongeze kasi ya kutekeleza mradi huu ili ukamilike kwa muda,” amesema Balozi Kallaghe.
0 Comments