Header Ads Widget

TRA MBEYA YAWATAKA WAWEKEZAJI NA WACHIMBAJI MADINI KULIPA KODI

 


Na Thobias Mwanakatwe, SONGWE


MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mbeya imewataka wawekezaji wa migodi,wafanyabiashara na wachimbaji wadogo wa madini kutambua wajibu wao wa kulipa tozo na kodi mbalimbali serikalini kwa ajili ya maendeleo yao na taifa kwa ujumla.


Afisa Elimu kwa Mlipa Kodi TRA Mkoa wa Mbeya,Godson Msukuru, ametoa wito huo leo (Oktoba 12, 2024) wakati wa maonesho dhahabu yanayofanyika kata ya Saza Wilaya ya Songwe Mkoa wa Songwe.


"Tunawaomba wanaojishughulisha na shughuli za madini walipe kodi kwa maendeleo ya nchi ili kuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ili serikali iweze kutekeleza miradi ya maendeleo," amesema Msukuru.


Msukuru amesema kodi hutozwa kwamujibu wa sheria ambapo TRA inaangalia shughuli za kiuchumi ambazo zinamuwezesha mtu kupata kipato ambazo ni biashara,ajira na uwekezaji.



Amesema maeneo hayo yanayohusika na utozaji kodi kwamujibu wa sheria ya mapato cap 337 ya mwaka 2004 ambapo katika sekta ya madini wapo waliowekeza kwenye migodi na wapo walioajiriwa ndani ya migodi ambapo wote wanapaswa kulipa kodi.


Msukuru ameongeza kuwa waliowekeza kwenye migodi wanatozwa kodi kulingana na uwekezaji waliowekeza ambapo wanatozwa kodi ya mapato wakati walioajiriwa kwenye migodi wanatozwa kodi ya mishahara ambayo ni kwamujibu wa kifungu cha 7 cha sheria ya mapato ya mwaka 2004.


Naye Afisa Kodi Msaidizi, Hafsa Mwindadi, amsema katika migodi wapo wanaolipa kodi vizuri na wapo wachache ambao ulipaji wao umekuwa sio mzuri pengine ni kutofahamu umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi.


Amesema kutokana na hali hiyo TRA imekuwa ikitoa elimu kwenye migodi na maeneo mbalimbali ili wanaopaswa kulipa kodi watambue umuhimu wake na baada ya elimu hiyo mwitikio umekuwa mkubwa.


"Ni katika mkitadha huo huo ndio maana leo hii unatuona TRA hapa tumekuja kushiriki maonesho ya dhahabu ambapo kwetu ni fursa nzuri kuwapa elimu wafanyabaishara,wawekezani na wachimba madini," amesema Hafsa.


Kwamujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Songwe,Solomoni Itunda, alisema maonesho ya dhahabu yatafanyika wilayani humo kuanzia Oktoba 12 hadi 14 mwaka huu.


Alisema maonesho hayo ambayo yameandaliwa na Mc Edwin Luvanda Branding and Entateiment Company, yatafuatiwa na tamasha litakalofanyika Oktoba 14, 2024 litakalofanyika mjini Chunya kwenye ukumbi wa Omari Hotel.





Mkuu huyo wa Wilaya alisema wakati wa maonesho hayo, wachimbaji wadogo,wa kati na wakubwa watapata fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu wa namna kufanya kazi za uchimbaji.


Aliongeza kuwa pia wakati wa maonesho hayo wachimbaji wataweza kuonyesha zana mbalimbali wanazozitumia katika shughuli za uchimbaji madini.


Itunda alisema kwenye tamasha yapo makundi mbalimbali ya wachimbaji ambayo yatapewa tuzo wakiwamo wachimbaji chipukizi na wachimbaji wanaolipa kodi kwa uaminifu serikalini.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI