Header Ads Widget

SERIKALI YAKEMEA MAPENZI YA JINSIA MOJA KWA WATUMISHI WA UMMA

 

NAIBU Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Xavier Daudi, amekemea vikali vitendo vya mahusiano ya jinsia moja miongoni mwa watumishi wa umma, akisema kuwa vitendo hivyo ni kinyume na maadili, mila, na desturi za Kitanzania. 


Daudi ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma katika kikao cha kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na utawala bora baina ya taasisi zinazohusika na usimamizi wa maadili ya utendaji na mamlaka zinazosimamia maadili ya kitaaluma.

Daudi amesema kuwa ofisi yake imeanza kupokea malalamiko na tuhuma kuhusu mmomonyoko wa maadili miongoni mwa watumishi wa umma, hususan vitendo vinavyohusiana na mahusiano ya jinsia moja. 

Ameeleza kuwa vitendo hivyo vinasababisha ukiukwaji mkubwa wa maadili kazini, jambo ambalo ni kinyume na mila za Kitanzania. 


"Tukumbuke kuwa si kila kitu kinachotoka nje ya nchi ni kizuri; jambo hili linatusumbua sana, mapenzi ya jinsia moja," alisema Daudi.

Na kuendelea kusema, "Fikiria unajihusisha na mahusiano hayo, unavuruga utaratibu mzima wa maadili katika taasisi. Tukumbuke, hili si jambo linalokubalika serikalini, hatuhitaji mambo ya hovyo kama hayo, na msimamo wa nchi upo wazi katika eneo hili."

Daudi pia alibainisha kuwa serikali imeanza kuchukua hatua dhidi ya watumishi wanaojihusisha na vitendo hivyo au wenye viashiria vya kufanya hivyo. 

Amesema kuwa kuwahamisha watumishi hao hakutatui tatizo, kwani wanapopelekwa sehemu nyingine wanaweza kuendeleza tabia hizo na kuharibu zaidi. 

"Tulikemee hili zaidi, kwani si sehemu ya maadili yetu katika taifa la Tanzania. Hata kama sehemu nyingine wanaona ni vitu vya kawaida, kwetu sisi hapana," amesisitiza.

Aidha, Daudi aliwataka viongozi wa taasisi za dini na jamii kuchukua hatua na kulikemea jambo hilo ili kulinda maadili ya taifa na kuhakikisha jamii inaendelea kuzaliana. 

"Tufikirie mara mbili, wananchi wameacha kuzaliana, na sisi pia tujifikirie huko tunakoelekea; tutakapoacha kuzaliana, baada ya miaka kadhaa wanaume wameamua kuolewa na wanawake wameamua kuoa. Tufikirie mara mbili na kila mmoja achukue nafasi yake, hasa taasisi za dini na jamii kwa ujumla," amesema.

Akizungumzia kikao hicho, Daudi alisema amefurahishwa na maandalizi ya kikao hicho, kwani kimekuja wakati muafaka na kimewaleta pamoja kada mbalimbali. 

Amesisitiza kuwa maadili ni jambo muhimu sana kwa watumishi wa umma na akaongeza kuwa baadhi ya watumishi hawajui mavazi yanayofaa kazini au kutumia lugha nzuri wanapotoa huduma.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi kutoka Idara ya Utumishi wa Umma Ally Gowe alisema kupitia kikao hicho wamepokea maelekezo na watajadili na washiriki ili kuja na maazimio yatakayosaidia kukabiliana na changamoto hiyo, ambayo ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeanza kupokea taarifa zake kutoka kwa wananchi na watu wenye nia njema na serikali.

"Kimsingi, vitendo hivyo ni kinyume na maadili yetu. Sasa kupitia kikao hiki tutatoka na maazimio, kwani tumeshapewa maelekezo ya nini tufanye katika kupambana na janga hili, " Amesema Gowo

 Na kuongeza "Ni muhimu pia kuongeza wigo wa sifa tunapochagua watumishi wapya, tuangalie zaidi tabia na mienendo yao mapema ili kubaini viashiria hivyo na kuchukua hatua kabla hawajaingia katika utumishi wa umma," Amesema 

Hata hivyo amesema Kwa wale tuliokwisha kupokea, tutakubaliana kupitia kikao hiki namna ya kutatua changamoto hiyo, hasa kwa wale wanaohitaji msaada wa kisaikolojia, kwani wapo ambao wako tayari kubadilika. 

Kuhusu kikao hicho, Daudi alisema Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ina majukumu mengi, mojawapo likiwa ni kusimamia maadili ya utendaji kwa watumishi wa umma. 

Amesema kuwa ofisi yake imekuwa na njia nyingi za kutekeleza jukumu hilo, mojawapo ikiwa ni kupitia vikao kazi vya wadau wa maadili, ambapo wanashirikiana na taasisi mbalimbali zinazohusika na maadili ya utendaji, kama vile TAKUKURU, Ofisi ya Ukaguzi wa Taifa, Tume ya Utumishi wa Umma, Tume ya Utumishi wa Walimu, Wizara ya Katiba na Sheria, na nyinginezo.

"Pia tunashirikiana na mamlaka za usimamizi wa maadili ya kitaaluma, bodi, na mabaraza yanayohusika na taaluma mbalimbali. Hawa ni wadau wakubwa, kwani tumekuwa tukibadilishana taarifa na uzoefu," amesema Gowo

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI