Na Ashrack Miraji Matukio Daima App
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu ameagiza vyombo vya usalama kuwatafuta watu wote waliohusika kuhujumu miundombinu ikiwemo vibanda vya kupumzikia watalii pamoja na mabomba ya maji katika hifadhi ya msitu asilia Chome (Shengena) wilaya ya Same mkoani humo.
Ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake alipoambatana na Kamati ya Usalama Wilaya ya Same ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mkuu wa Wilaya hiyo Kasilda Mgeni, baada ya kupata taarifa za uharibifu kwenye Hifadhi hiyo chini ya Wakala wa huduma za Misitu Tanzania (TFS) akisisitiza agizo lake wahusika kuapatikana ndani ya siku saba
“Nimesikitishwa sana na baadhi ya watanzania ambao bado hawatambui kwamba hii mali ni ya kwao, kwenye hili eneo kuna manzari mazuri, kuna sehemu za kupumzika na kunapendeza kabisa, sasa wanatoka watanzania wachache wanakwenda kuvunja mali ya Serikali…, hatuwezi kuvumilia vitendo vya namna hii”. Alisema RC Babu.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amepiga marufuku kwa wachimbaji wadogo wa madini kuingia kwenye hifadhi hiyo na kuendesha shughuli za kibinadamu ikiwemo uchimbaji wa madini bila vibali na kusisitiza Serikali haitasita kuchukua hatua kwa watakaobainika kukiuka miongozo na sheria za uhifadhi kwakuwa eneo hilo ni mahususi kwa shughuli za Utalii na utunzaji wa mazingira.
Sanjari na suala hilo RC Babu ametembelea pia kaya za wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF) kuona hali ya utekelezaji wa miradi hiyo ambayo Serikali huzipatia fedha baadhi ya kaya ambazo zimeingizwa kwenye mpango huo kwa lengo la kuziinua kiuchumi kutokana na sababu mbalimbali zinazo wakabili kwenye jamii.
0 Comments