Kalani wa Kituo Cha chuo Cha Afya mjini Iringa Veronica Mbeya akimuandikisha Mwananchi wa mtaa wa Sabasaba kata ya Gangalonga ambae ni mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa (NEC)Salim Abri Asas Jana picha na Matukio Daima media
NA MATUKIO DAIMA MEDIA
WAKATI zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la Mpiga kura likiwa limefunguliwa Rasmi kwa Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan Kuongoza zoezi la kujiandikisha Kitaifa ili kushiriki chaguzi wa serikali za mitaa tukio ambalo ni muhimu sana katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata fursa ya kuchagua viongozi wanaowakilisha maslahi yao kwa karibu zaidi.
Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa (NEC) Salim Abri Asas ameongoza zoezi hilo kwa Wana CCM mkoa wa Iringa kwenda kujiandikisha katika Kituo Cha chuo Cha Afya Kituo Cha mtaani kwake .
Ikumbukwe kuwa Kwa mwaka huu, uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Novemba 27, na ni muhimu kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kushiriki kikamilifu katika mchakato huo wa kidemokrasia.
Kwani Kuna umuhimu mkubwa wa Kujiandikisha na Kushiriki Uchaguzi huo .
Asas anasema ni haki ya Kidemokrasia Kila raia mwenye sifa za kupiga kura kushiriki kwani anayo haki ya kikatiba ya kushiriki katika uchaguzi.
Kuwa kujiandikisha ni hatua ya kwanza ya kuhakikisha kuwa haki hiyo inatimizwa.
Asas anasema kuwa bila kujiandikisha mtu hawezi kushiriki katika mchakato wa uchaguzi na hivyo kupoteza fursa ya kuchagua viongozi wa ngazi za chini kama vile wenyeviti wa vijiji na mitaa, ambao ni muhimu katika maendeleo ya kila siku ya jamii.
Amesema kuwa Uchaguzi wa Serikali za mitaa ndio chombo cha kwanza cha kusimamia maendeleo ya jamii.
Kwani anasema viongozi wanaochaguliwa katika ngazi hizi hutoa maamuzi yanayoathiri moja kwa moja maisha ya wananchi.
"Hawa ndio wanaoamua juu ya matumizi ya rasilimali za mtaa, mipango ya maendeleo, na utekelezaji wa miradi mbalimbali kama vile barabara, shule, vituo vya afya, na huduma za kijamii"
Hivyo ushiriki wa wananchi katika uchaguzi unawapa nguvu ya kuchagua viongozi bora watakaosukuma maendeleo yao.
Kama alivyobainisha Salim Asas kuwa vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kushiriki uchaguzi.
" Vijana ni chachu ya mabadiliko na maendeleo katika jamii, na wanapaswa kutumia fursa ya kujiandikisha na baadaye kushiriki katika uchaguzi ili kuhakikisha kwamba wanachagua viongozi wenye maono yatakayokuza ajira, elimu, na fursa nyingine za kiuchumi zinazowahusu"
Anasema kuwa kupiga kura ni njia mojawapo ya kuwafanya viongozi wawajibike, Wananchi wanapopiga kura, wanakuwa na sauti ya kuchagua viongozi wanaoamini watasimamia vyema rasilimali za mtaa na kutekeleza miradi yenye tija kwa jamii. Pia, kupitia uchaguzi, wananchi wanaweza kuwaondoa madarakani viongozi wasiofaa.
Anasema kuwa uchaguzi hutoa nafasi ya kujenga mshikamano wa kitaifa na amani.
Hivyo wananchi wanaposhiriki kikamilifu katika uchaguzi, wanachangia kupunguza migogoro ya kisiasa na kijamii kwa kuwa na viongozi wanaochaguliwa kwa njia za kidemokrasia.
"Amani na utulivu ni misingi ya maendeleo endelevu, hivyo ni muhimu kuhakikisha kila mmoja anashiriki"anasema
Kuhusu uhamasishaji makundi maalumu wakiwemo watu wenye Ulemavu alisema CCM kinatambua makundi yote na umefanyika uhamasishaji mkubwa kuona Kila mmoja anashiriki kujiandikisha .
Hata hivyo alisema Chama kinaimani kubwa ya kuendelea kushinda kwenye chaguzi mbali mbali kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kujenga miradi mikubwa Kila Kona ya nchi hii.
Hivyo anasema ili serikali kuendelea kutekeleza Miradi hiyo na ili Kila Mwananchi mwenye sifa aweze Kuchangua viongozi watakaoshirikiana na Rais Dkt Samia Kuleta maendeleo ni vizuri kushiriki Uchaguzi huo kwa kuanza na kujiandikisha .
Kheri James ni mkuu wa wilaya ya Iringa amewataka watumishi wote na wananchi wa Iringa kujitokeza kwa wingi kwenda kujiandikisha .
Yusuph Nyagawa ni mwenyekiti mstaafu wa serikali ya mtaa wa Sabasaba anasema kuwa katika mtaa wake umefanyika uhamasisisha mkubwa hivyo Imani yao wananchi wengi kushiriki Uchaguzi huo.
Ifahamike kuwa kujiandikisha na kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa si tu ni haki ya kidemokrasia, bali ni wajibu wa kila raia.
Ni fursa ya kipekee kwa wananchi kuamua mustakabali wa maeneo yao na kuchagua viongozi watakaosimamia maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Hivyo kila raia mwenye sifa za kupiga kura anapaswa kujiandikisha na kuhakikisha kuwa anashiriki kikamilifu katika uchaguzi ujao utakaofanyika Novemba 27 mwaka huu.
Mwisho
0 Comments