Na Matukio Daima media
UTENDAJI kazi na uwajibikaji mzuri wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan umeendelea kuwavutia watanzania walio wengi na hata baadhi yao Kutamani azidi Kuongoza kipindi kingine Cha Miaka mitano kinachoanza mwaka 2025.
Matumaini haya ni chachu kwa wale wanaomsaidia Rais Dkt Samia Suluhu Hassan nao kuendelea kutimiza vema wajibu wao kuwa wasaidizi wa kweli ili Imani izidi zaidi kwa wananchi .
Ikumbukwe kuwa tangu kuapishwa kwake mnamo Machi 19, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan ameandika historia isiyofutika, si tu kwa kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza Tanzania, bali pia kwa mafanikio makubwa katika nyanja za uchumi, diplomasia, na maendeleo ya kijamii.
Uongozi wake umeleta mabadiliko chanya ambayo yamevutia hisia za mataifa ya nje, huku yakitoa fursa mpya kwa Watanzania katika sekta mbalimbali.
Hali hii imethibitisha kwamba Tanzania iko katika njia sahihi ya maendeleo, na zawadi pekee kutoka kwa wananchi ni kumwunga mkono Rais Samia katika safari ya Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Aidan Mlawa ni mdau wa maendeleo wilayani Kilolo mkoani Iringa anasema kuwa Rais Samia amekuwa kinara wa kuboresha uchumi kwa kuendeleza miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR), barabara kuu, na maboresho ya bandari.
Anasema kuwa juhudi zake katika kuhakikisha uzalishaji wa umeme wa uhakika kupitia mradi wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) ni mfano wa dhamira yake ya kuweka misingi ya uchumi wa viwanda.
"Sera za uboreshaji wa mazingira ya biashara zimechangia kuimarika kwa uwekezaji wa ndani na nje, hali ambayo imefungua nafasi nyingi za ajira kwa vijana".
Mlawa anasema kuwa Rais Samia ameimarisha pia sekta ya kilimo kupitia mpango wa “Agenda 10/30,” lengo likiwa kuongeza uzalishaji na usalama wa chakula ifikapo mwaka 2030.
Katika kipindi kifupi cha uongozi wake, Rais Samia ameimarisha uhusiano wa kidiplomasia na mataifa mbalimbali, hatua iliyosaidia kuongeza uwekezaji wa kigeni na kuboresha taswira ya Tanzania kimataifa. Ziara zake katika mataifa kama Marekani, Uingereza, na nchi za Afrika zimechangia kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na kisiasa, huku zikileta mikataba yenye tija kwa taifa.
Akitolea mfano anasema ushirikiano wake na mashirika ya kimataifa umesaidia kufanikisha miradi ya maendeleo katika sekta za afya, elimu, na mazingira.
Kuwa Rais Samia ameonyesha uongozi wa kidiplomasia unaojikita katika usuluhishi wa migogoro na kulinda amani, akitoa mchango mkubwa katika jumuiya za kikanda kama Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na SADC.
"Uongozi wa Rais Samia umeonyesha kujitolea katika kukuza demokrasia kwa kufungua milango ya majadiliano na vyama vya siasa vya upinzani."
Hivyo kupitia juhudi hizi, maridhiano yameboreshwa, na hali ya siasa imekuwa ya utulivu zaidi.
Anasema kuwa Rais Samia ameonyesha kwamba demokrasia siyo uhasama bali ushirikiano wa kuijenga Tanzania yenye neema.
Aidha anasema uhuru wa vyombo vya habari na kutoa nafasi kwa wananchi kushiriki katika maamuzi yanayohusu ustawi wa taifa.
Kuwa hii ni ishara kwamba uongozi wake unaheshimu haki za msingi za binadamu na kuimarisha misingi ya amani na utulivu.
Pamoja na mafanikio makubwa, Rais Samia anakabiliwa na changamoto kadhaa, kama vile mfumuko wa bei za bidhaa na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Hata hivyo, hatua za kupunguza mzigo wa maisha kwa wananchi kupitia ruzuku kwenye mafuta na kuwekeza kwenye kilimo endelevu zinaonyesha kwamba serikali yake ina maono na mikakati madhubuti.
Kuna pia changamoto za kisiasa, hasa kutoka kwa baadhi ya makundi ya upinzani ambayo yanashiriki katika kampeni za uchochezi badala ya kutoa mawazo mbadala ya maendeleo. Hii inadhihirisha umuhimu wa kuwa na upinzani wenye tija unaojikita katika kujenga, si kubomoa.
Amani ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya taifa lolote, na Tanzania imebarikiwa kuwa na utulivu wa kisiasa na kijamii kwa miaka mingi.
Aidan Mlawa, mdau wa maendeleo kutoka Kilolo aliyesomeshwa kwa pipa la pombe anasisitiza kuwa upinzani ni sehemu ya demokrasia, lakini hauna nafasi pale unapoendekeza vurugu na kuchochea migawanyiko miongoni mwa wananchi.
Badala yake, Mlawa anahimiza Watanzania kuendeleza mshikamano na kushirikiana na serikali katika kujenga taifa lenye mafanikio.
Rais Samia ameweka mfano mzuri wa jinsi uongozi wa maridhiano na mshikamano unaweza kufanikisha malengo ya kitaifa.
Anasema Rais Samia ameonesha ushirikiano kati ya sekta za umma na binafsi umeimarika, na juhudi za kuwashirikisha wananchi katika mipango ya maendeleo zimeongeza uwajibikaji wa pamoja kwa maslahi ya taifa.
Hivyo amesema Wakati huu Uchaguzi mkuu wa 2025 unapokaribia, ni dhahiri kwamba Rais Samia anaungwa mkono na Watanzania wengi kutokana na mafanikio yake.
"Uongozi wake umeonyesha dira na maono ya mbali, huku akifanya mageuzi katika sekta zote muhimu, Amani, maendeleo, na ushirikiano wa kidiplomasia alioujenga vinaashiria uongozi wa aina ya kipekee unaostahili kuendelea"anasema Mlawa
Aidha anasema kuwa hakuna sababu ya kuendeleza upinzani usio na tija, bali ni vema kwa wananchi kuungana na kumuunga mkono Rais Samia ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.
Anasema maendeleo hayana chama, na mafanikio ya Rais Samia ni ushindi wa kila Mtanzania.
"Rais Samia Suluhu Hassan ameonyesha mfano bora wa uongozi unaojali maslahi ya taifa na kuweka mbele ustawi wa wananchi".
Kuwa Rais Samia ametengeneza mazingira rafiki ya maendeleo, kufanikisha diplomasia yenye manufaa, na kuhakikisha demokrasia na utawala bora vinaimarika.
Kuwa mbali ya changamoto zilizopo, Tanzania ipo katika mkondo sahihi wa mafanikio.
Joshua Ndelwa mkazi wa Ilula na Amina Alli mkazi wa Image wanasema kuwa wanaungana na Mlawa kuona Rais Samia anaendelea kuungwa mkono kwenye Uchaguzi mkuu Ujao .
Huku Deus Sanga mkazi wa Iringa mjini na Maria Sanga wanasema kuwa wanajivunia mafanikio haya kwa kumwunga mkono Rais Samia katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Kuwa Kama alivyosema Mlawa, upinzani wa kweli ni ule unaojenga, si kuvuruga.
Wanasema watanzania wanapaswa kushirikiana kwa amani na mshikamano, kuhakikisha Tanzania inazidi kung'ara katika ramani ya dunia badala ya kuwasikiliza wanaohamasisha Vurugu.
0 Comments