Na Matukio Daima media
RIGATHI Gachagua amekua Naibu Rais wa kwanza nchini Kenya chini ya Katiba mpya iliyopitishwa mwaka 2010 na wa pili mwenye hadhi yake kuondolewa madarakani.
Kabla ya Katiba ya Kenya kubadilishwa, cheo cha Naibu Rais kilifahamika kama Makamu Rais na wa kwanza kuondolewa ofisini kwa kupigiwa kura ya kutokua na imani alikuWa marehemu Dkt. Josephat Karanja wakati wa utawala wa Hayati Rais Daniel arap Moi.
Enzi za marais watatu waliotangulia, Mzee Jomo Kenyatta, Moi na Mwai Kibaki, Katiba iliwaruhusu kuteua Makamu Rais baada ya uchaguzi, hivyo alikuWa na uwezo wa kumtimua muda wowote au Bunge kupiga kura ya kutokuWa na Imani na Makamu Rais.
Lakini kwa Katiba mpya, muwaniaji kiti cha urais anatakiwa kuteua mgombea mwenza na hawezi kumtimua ila hilo linaweza kufanikishwa endapo Bunge litapiga kura ya kutokuwa na imani naye au madaktari wakathibitisha hayuko vizuri kiafya na kiakili au kujiuzulu au kifo.
Gachagua ambaye amekuwa mmoja wa watu waliosimama na Ruto kipindi anapitia wakati mgumu akiwa Naibu Rais chini ya utawaka wa Rais Uhuru Kenyatta, amejikuta uhusiano wake na Rais Ruto umedorora kwa miezi ya hivi karibuni.
Ilihitajika neno moja tu kutoka kwa Rais Ruto kumnusuru aliyekuwa naibu wake kuepuka kuondolewa madarakani na wabunge, lakini ukimya wa kiongozi huyo mkuu wa nchi ilikuwa ishara tosha amebariki wabunge wa mabunge wote mawili – Bunge la Taifa na Seneti – kutumia Kifungo cha 145 ya Katiba ya Kenya kumtimua ofisini Gachagua.
Hata hivyo, namna ya zoezi hilo lilivyopelekwa haraka haraka huku mashitaka 11 yakiwasilishwa dhidi ya Gachagua ndiyo yamewashangaza Wakenya wengi.
Kupanda ngazi hadi kuwa Naibu Rais nalo pia liliwashangaza wengi wakimuona kama mtu ambaye bado hajakomaa kwa wadhifa huyo mkubwa ikizingatiwa alikuwa msaidizi binafsi wa Rais Mstaafu Uhuru, kisha akahudumu kama Mbunge wa Mathira iliyopo Kaunti ya Nyeri kwa muhula moja wa miaka mitano kabla ya kuapishwa kuwa Naibu Rais.
Uteuzi wa Gachagua kuwa mgombea mwenza kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 uliibua mjadala huku taarifa ndani ya kikao cha Chama cha United Democratic Alliance (UDA) zikisema chama hakikumpendekeza kuwa mgombea mwenza.
Inasadikiwa wanachama wa UDA walimtaka Profesa Kithure Kindiki aliyekuja kuteuliwa Waziri wa Usalama na moja wa mawakili mahiri waliomtetea Rais Ruto wakati akikabiliwa na mashitaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu jijini Hague, Uholanzi kuwa mgombea mwenza.
Ila inasemekana vitisho vya Gachagua na pia fedha alizotumia kusimamisha chama cha UDA ndiyo iliyowafanya wanachama kumkubali shingo upande.
Kauli zake baada ya kuapishwa nazo zilimponza na kujikuta akitengeneza uadui sio tu na upinzani chini ya uongozi wa Raila Odinga mbali hata pia ndani ya serikali.
Mara kadhaa alitumia majukwaa ya kisiasa kumshambulia kwa maneno makali Rais Mstaafu Uhuru na kujitwisha ‘ufalme’ wa Mlima Kenya licha ya watu wengi kutoka eneo hilo wakimtambua Uhuru kama kiongozi na msemaji wao hadi atakapopendekeza mrithi wake.
Kujipiga kifua kwa Gachagua ikiwa ni ishara ya kujiandaa kumrithi Rais Ruto atakapostaafu baada ya mihula miwili, kuliibua mpasuko miongoni mwa wanasiasa kutoka Mlima Kenya inayoundwa na jamii tatu kuu; Wakikuyu, Waembu na Wameru.
Profesa Kindiki ni mtu kutoka jamii ya Wameru ambao wanahisi tonge lilipokonywa mdomoni mwao na Gachagua hivyo kutimuliwa ofisini kwa Gachagua ilikua njia nyeupe na hususan chaguo rahisi ya Ruto kupendekeza jina la Kindiki kuwa Naibu Rais mteule.
Nje ya watu kutoka Mlima Kenya, kauli ya Gachagua hususan ya kuifananisha Serikali na kampuni na kwamba wanaopaswa kufaidi ni wenye hisa akimaanisha waliowapigia kura, iliwakera watu kutoka jamii zingine na kumuona hana sifa ya kuwa Naibu Rais.
Bosi wake, Rais Ruto, hakufurahishwa na kauli hii akisisitiza kila Mkenya pasipo kujali mirengo yao ya kisiasa anapaswa kupelekewa maendeleo na nyufa baina ya viongozi hawa wawili wakuu zikaanza kudhihirika alipoondoa baadhi ya majukumu ya Naibu Rais na kumkabidhi Mkuu wa Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, Musalia Mudavadi.
Rais Ruto ambaye alisema hatoruhusu madhila yaliyomkuta katika muhula wa mwisho wa utawala wa Rais Uhuru wakati huo yeye akiwa Naibu Rais yamkute naibu wake Gachagua, aliamua kunyamza mawaziri walipokuwa wanamuonyesha dharau.
Waziri wa Ulinzi, Aden Duala, alikuwa moja ha wao mawaziri ambapo alitoa agizo kwamba hakuna kiongozi yoyote wa serikali ikiwemo Naibu Rais anaruhusiwa kutumia ndege ya jeshi isipokua Rais pekee yake.
Gachagua ambaye alijitetea kwamba yeye kama ilivyokua Rais Ruto alichaguliwa na Wakenya milioni 7.2, ilipingwa vikali na Waziri Duale akimshutumu Gachagua kwa kujaribu kusaka huruma za wananchi na kusisitiza aliteuliwa na Ruto kuwa mgombea mwenza.
“Inasikitisha kuona mtu ambaye alikua Naibu Rais sio kupitia uchaguzi wa moja kwa moja bali kutokana na uteuzi wa Rais, akijigamba kuchaguliwa na mamilioni,” Duale alisema.
Gachagua anaondoka ofisini baada ya kuhudumu kwa takribani miaka miwili huku kimbilio lake la mwisho kunusuru kibarua chake ikiwa ni mahakama akifanikiwa kupata amri ya mahakama kuzuia mchakato wa upatikanaji wa mrithi wake hadi kesi itakapotajwa Alhamisi Oktoba 24 mwaka huu.
Awali Bunge liliidhinisha jina la Profesa Kindiki kuwa Naibu Rais Mteule wadhifa aliyostahili wakati wa mchakato ndani ya chama cha UDA kusaka mgombea mwenza wa Ruto lakini Gachagua akatumia ubabe ‘kujimilikisha’.
Tofauti na Gachagua, Profesa Kindiki ambaye ni mwanasheria kitaaluma ni mtendaji zaidi kuliko kuongea, mtu makini na mwenye sura ya kitaifa.
Akihudumu katika wadhifa wake kama Waziri wa Usalama, alikuja na mikakati iliyopelekea visa vya uhalifu hususan eneo la Bonde la Ufa kupungua na pia kuleta mabadiliko yenye tija ndani ya idara za polisi.
Karibu kutangaza na Matukio Daima media tunapokea matangazo aina mbalimbali kwa gharama poa piga 07540262099
0 Comments