NA JOSEA SINKALA, SONGWE.
Mkuu wa wilaya ya Songwe Mhe. Solomon Itunda, amemkabidhi nyumba mama mmoja (58) mkazi wa Saza wilayani humo baada ya kujengewa na jirani yake ambaye alidaiwa kuingilia eneo lake bila makubaliano.
Wawili hao waliingia katika mgogoro miaka miwili iliyopita, hii ni baada ya mama huyo aliyejitambulisha kwa jina la Justina Mwangomo, kusafiri nje ya makazi yake kwenda kumuuguza ndugu yake ndipo aliporudi alikuta jirani yake akiendelea na ujenzi hadi kwenye eneo lake.
Kutokana na mgogoro huo wa kimipaka walifikishana kwenye Serikali huko Kibaoni kata ya Saza bila mafanikio na baadaye kwenda mkoani mjini Vwawa ambapo akiwa na nyaraka alishauriwa kurudi wilayani ambao walianza kushughulikia ombi lake hata kufanikiwa kutatuliwa.
Akisimulia kisa hicho mama huyo anasema "Ninakushukuru sana mkuu wa wilaya (Solomon Itunda Dc Songwe) kwani umeniandalia kaburi, baada ya kaburi la kuzikwa hili ni kaburi la kuishi yaani umenifunika ndio maana huwa wanasema hujui atakayekuzika. Wewe hunijui na mimi sikujui lakini umehakikisha nimepata nyumba, Mungu akubariki siku zote kila unapokanyaga Mungu akutangulie", ameeleza mama huyo akimshukuru mkuu wa wilaya ya Songwe.
Mama Justina Samweli Mwangomo (58) mkazi wa Saza Songwe katika mazungumzo yake na kituo hiki amesema licha ya kwamba eneo lake la awali lilikuwa kubwa kuliko alilonunuliwa na kujengewa nyumba amekubali kwasababu amepata eneo la kuishi na kumwachia jirani yake eneo la awali ambaye ndiye alinunua eneo lingine na kumjengea nyumba ya vyumba vinne na choo.
Akizungumza kabla ya kumkabidhi nyumba hiyo, mkuu wa wilaya ya Songwe Mhe. Solomon Itunda, amezishukuru familia hizo mbili kwa kukaa meza moja ya mazungumzo na kuamua kumaliza mgogoro huo bila ugomvi.
"Ndugu zangu baada ya kesi hii kufika ofisini kwangu tulianza kuishughulikia na namshukuru Yohana ambaye alikuwa mdaiwa alitumia busara akakubali kutafuta eneo lingine na kujenga nyumba kwa ajili ya huyu mama halafu yeye abaki kwenye eneo lile la kwanza na kwakuwa walikubaliana mimi nashukuru na hii ni kupitia mpango wetu wa kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua", ameeleza mkuu huyo wa wilaya.
Hata hivyo ametoa wito kwa wananchi wake kujenga utamaduni wa kukaa meza ya mazungumzo kunapokuwa na tofauti baina yao katika jamii badala ya kuchukua hatua zisizo sahihi ikiwemo kuuana na kujiingiza kwenye imani za kishirikina.
Aliyekuwa mdaiwa wa eneo hilo ambalo halijatajwa ukubwa kijana Yohana Brithon, ameshukuru ofisi ya wilaya kwa upatanishi pamoja na familia ya mama huyo kukubali kumaliza mgogoro huo kwa kujengewa nyumba eneo lingine kutokana na mgogoro wa mpaka.
Sanjari na hayo yote, mkuu wa wilaya ya Songwe mkoani Songwe Solomon Itunda, ameagiza mthaminishaji ardhi Halmashauri ya Songwe kwenda kupima na kumpatia hati ya ardhi mama huyo bila kumtoza gharama zozote.
0 Comments