Na Mwandishi Wetu
Makamu wa kwanza wa rais Othman masoud amekitaka chama cha wanasheria Zanzibar (ZLS) kusimama imara kutetea haki za wananchi zinapovunjwa hasa katika kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Tamko hilo amelitoa wakati akifunguwa mkutano mkuu wa mwaka chama hicho uliofanyika visiwani Zanzibar na kumchagua Joseph Shabani Magaza kuwa rais wa chama hicho.
Alisema wananchi wanapokosa haki zao chama cha wanasheria kinapaswa kiwe kimbilio lao ili kuhakikisha haki zao zinalindwa kwa mujibu wa katiba na sheria.
“Chama cha wanasheria pale katiba ya nchi inapovunjwa na mtu au mamlaka yoyote, chama kinastahiki kiwe mstari wa mbele kupaza sauti na kuchukua hatua stahiki dhidi ya uvunjaji huo”alisema Othman.
Aidha alisema chama hicho kinawajibu wa kulinda haki za kiraia ikiwemo kusimamia mashauri yenye maslahi ya umma ili kufikia misingi ya utawala bora.
“Ni kinyume na ni fedheha kubwa pale haki za kiraia zinapokuwa hatarini ama kwa sababu ya wenye mamlaka au maslahi ya kibiashara, sio vyema kwa chama cha wanasheria kuwa kimya na kutotimiza wajibu wa kupaza sauti tukifika hapo raia hawatakuwa na mlinzi madhubuti dhidi ya matumizi mabaya ya madaraka, kukosa uwajibikaji, ufisadi na dhulma za kimfumo au kiutendaji”alisema Makamu wa kwanza huyo.
Othman alisema wananchi wengi Zanzibar wanakosa haki zao hasa haki ya ardhi, kuchaguwa na kuchaguliwa wanaponyimwa haki zao kwa wenye mamlaka kutofuata sheria ama kutumia vibaya sheria jambo ambalo ni kinyume na katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Aidha aliwataka wanasheria kutenga muda maalum kwa ajili ya kutoa elimu ya uraia na msaada wa kisheria pale wananchi wanapokuwa na matatizo na kukoseshwa haki zao.
Othman alisema wanasheria wanayo nafasi kubwa katika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia ushauri wao muhimu wa kisheria sambamba na kuhakikisha makubaliano na mikataba inazingatia sheria na kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima na hivyo kusaidia kujenga ustawi bora wa jamii yenye umoja na mshikamano.
Akizungumzia uchaguzi mkuu wa 2025, Othman alisema, uchaguzi sio wa chama na wala si suala la kuamua masuala ya kisiasa bali ni mahkama ya wananchi ambapo wanapata fursa kuamua hatma ya nchi yao.
“Watu wanaochaguliw ndio watakuja kutunga sio sheria tu bali hata kurekebisha katiba ya nchi, ndio watakaoweka viwango vya kodi, ndio watakaochagua majaji na mahakimu, ndio wataoweka sera na miongozo, ndio watakao kuwa na dhamana ya kutumia fedha na rasilimali zote za nchi. Ndio watakaoamua vipaombele vya nchi na ndio watakaokuwa na mamlaka ya kukulinda au kukuacha bila ya ulinzi unaostahiki”alisema.
Alisema kwa mujibu wa katiba na sheria wananchi wote wanahaki ya kuchagua au kuchaguliwa na kutaka mamlaka dhamana kuhakikisha haki inatendeka katika uchaguzi huo.
Waziri wa katiba, sheria na utawala bora, Haroun Ali Suleiman aliwataka wanasheria kufuata maadili ya kazi zao kwa kutenda haki na kujenga imani na serikali na hakuna tatizo katika kuikosoa ama kuishauri serikali.
Alisema serikali inaendelea na kazi kubwa ya kuimarisha serikali ya umoja wa kitaifa na kuwataka wanasheria kuunga mkono juhudi hizo ili kujenga umoja wa kitaifa kwa wananchi wa Zanzibar.
Naye aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Masoud Rukazibwa, alisema wanakabiliwa na vikwazo vingi ikiwemo kukosa fursa ya kupewa kazi na serikali za kusimamia mikataba katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alisema pia wanakabiliwa na changamoto ya upungufu wa rasilimali hususan katika maeneo ya vijijini ambako huduma za kijijini bado zinahitaji sana.
Aidha alilalamikia hatua za wanasheria wa serikali kufanya kazi za uwakili kwa kutoza gharama ndogo jambo linalochangia kuharibu kazi ya uwakili hasa kwa vile wanasheria waserikali hawapaswi kufanya kazi za uwakili wa waaina hiyo
0 Comments