Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima App, Dodoma
TANZANIA inaendelea kutekeleza mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) kama sehemu ya mkakati wa kufanikisha uchumi wa kati ifikapo 2025.
SGR inachukuliwa kama nyenzo muhimu katika kukuza uchumi wa taifa kwa kupunguza gharama na muda wa usafiri wa abiria na mizigo, hivyo kuboresha huduma za kijamii na usafirishaji.
Mradi wa SGR umeleta ajira za moja kwa moja kwa watu 8,265, huku ukinufaisha wananchi wanaohusika moja kwa moja katika ujenzi wake.
Zaidi ya hayo, viwanda vya ndani vimepata faida kupitia ongezeko la mahitaji ya saruji, nondo, na vifaa vingine vya ujenzi, hali inayochangia kukuza pato la taifa.
Katika ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro, zilitumika nondo kilo milioni 45 na mifuko ya saruji milioni 3, huku kipande cha Morogoro hadi Makutupora kikihitaji nondo kilo milioni 70 na mifuko ya saruji milioni 6.4. Ongezeko hili la mahitaji limeimarisha sekta ya viwanda na kuhamasisha ushirikiano wa kiuchumi nchini.
Kwa kutumia umeme badala ya dizeli, SGR inatarajiwa kupunguza gharama za usafirishaji kwa asilimia 40%, hivyo kuongeza ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam.
Reli hii inaweza kubeba mzigo wa tani 10,000 kwa wakati mmoja, sawa na malori 500, hatua itakayopunguza msongamano barabarani, ajali, na gharama za usafiri.
Mradi huu pia umeimarisha sekta za kilimo, biashara, na viwanda.
Wakulima na wafanyabiashara wanapata fursa ya kusafirisha bidhaa zao kwa haraka na gharama nafuu, hali inayoongeza uwekezaji na maendeleo ya kiuchumi vijijini na mijini.
Kutokana na uboreshaji wa miundombinu ya reli, usafiri wa abiria na mizigo umekuwa rahisi.
Safari kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro sasa inachukua saa 1 na dakika 15, huku safari ya Dar es Salaam hadi Dodoma ikichukua saa 3 pekee.
Hii imepunguza changamoto za usafiri kwa wafanyabiashara na kuimarisha shughuli za kiuchumi.
Tanzania ina mifumo miwili mikubwa ya reli TRC – Kilomita 2,715 nchini,TAZARA – Kilomita 970 ndani ya Tanzania, sehemu ya reli yenye urefu wa kilomita 1,860 kutoka Dar es Salaam hadi New Kapiri-Mposhi, Zambia.
TRC inamilikiwa na Serikali ya Tanzania, huku TAZARA ikimilikiwa kwa usawa na Tanzania na Zambia.
Reli hizi zinaunganisha mikoa 14 na nchi jirani kama Zambia, Rwanda, Burundi, DRC, na Kenya, zikiimarisha mtandao wa usafiri wa kikanda.
Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inaweka mkazo kwenye ujenzi wa miundombinu ya reli kupitia mradi wa SGR. Mipango ya ujenzi inajumuisha:
Makutupora – Tabora (294 km)
Tabora – Isaka (130 km)
Isaka – Mwanza (250 km)
Tabora – Kigoma (411 km)
Mtwara – Songea – Mbamba-bay (1,000 km)
Pia kuna mpango wa kuanzisha reli ya jiji la Dodoma na kuboresha huduma za TAZARA.
Vifaa vya reli kama vichwa vya treni na mabehewa yanakarabatiwa na kununuliwa ili kuongeza ufanisi wa usafiri wa abiria na mizigo.
Mwandishi wa makala hii alizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ambaye alisema zaidi ya watu 900 hadi 1,000 wamenufaika moja kwa moja na mradi huu.
Senyamule alieleza kuwa usafiri wa SGR umekuwa mkombozi kwa wafanyabiashara na wasafiri, wakiwemo vijana na akina mama wanaojihusisha na biashara ndogo ndogo kama uuzaji wa zabibu na huduma za bodaboda na bajaji.
Mradi wa SGR pia umefungua fursa kwa wakandarasi wazawa na wafanyabiashara wa ndani.
Zaidi ya wazabuni 500 wanashiriki katika mradi huu, wakiwemo 15 waliopata kandarasi kubwa, huku wakiwa wamepata mafunzo ya kitaalamu.
Fursa hizi zimeongeza ujuzi wa wakandarasi wa ndani na kusaidia kuimarisha maendeleo ya kijamii.
Madereva wa bodaboda katika Stesheni ya Mkonze walieleza kuridhika kwao na mradi wa SGR.
Katibu wa umoja wao, Chacha Marwa, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuboresha miundombinu, hali inayowawezesha kujipatia kipato cha uhakika.
Zena Chitwanga, mfanyabiashara wa nguo kutoka Dodoma, alisema:
"SGR imekuwa mkombozi. Zamani safari zilichukua siku kadhaa, lakini sasa, naweza kufika Dar es Salaam na kurudi haraka."
Mradi wa SGR unatekelezwa kwa awamu tano, ukianzia Dar es Salaam hadi Mwanza, Tabora, na Kigoma.
Reli hii itaunganisha Tanzania na nchi jirani kama Uganda, Rwanda, na DRC, hivyo kuongeza fursa za biashara na usafirishaji wa mizigo kikanda.
Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa, alieleza kuwa safari ya majaribio kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ilikuwa mafanikio makubwa.
Kadogosa aliongeza kuwa ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro umefikia asilimia 98.93, na mradi wote una thamani ya dola bilioni 10.016.
Bahati Sweya, mkazi wa Chidachi, alieleza furaha yake:
"Usafiri wa SGR ni wa haraka na wa kuvutia. Tunapopita kwenye mahandaki, ni kama utalii wa ndani!"
Ikumbukwe kuwa mradi wa SGR unaleta mapinduzi katika sekta ya usafirishaji nchini Tanzania.
Hivyo kwa kuunganisha mikoa na nchi jirani, reli hii inafungua fursa mpya za biashara, inapunguza gharama za usafiri, na inakuza uchumi.
Ni wazi Mradi huu ni mchango muhimu katika safari ya kufanikisha uchumi wa kati ifikapo 2025.
0 Comments