Header Ads Widget

MAFANIKIO YA HIFADHI YA TAIFA YA RUAHA..



Na Matukio Daima media

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Godwell Ole Meing'ataki, ameweka wazi mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya hifadhi hiyo katika kipindi cha miaka 60 tangu kuanzishwa kwake.

 Akizungumza katika  kipindi Cha Tanzania ya Leo kilichorushwa na chanel ya Matukio Daima Tv Ijumaa asubuhi ,Meing'ataki alibainisha kuwa zaidi ya shilingi bilioni 60 zimewekezwa katika uboreshaji wa miundombinu, hatua ambayo imechangia ongezeko la watalii.

Miundombinu Bora Inayochochea Utalii

Alieleza kuwa uwekezaji huo umesaidia sana kujenga na kuboresha miundombinu ya msingi kama nyumba za wageni, nyumba za watumishi, na nyumba za madereva wanaoambatana na wageni. Uwepo wa miundombinu hii imeboresha hali ya kupokea wageni, ambapo awali, wageni walikabiliwa na changamoto nyingi za malazi, hasa madereva.

“Kwa sasa, kuna ujenzi wa cottages kwa ajili ya familia pamoja na hosteli mpya yenye uwezo wa kuhudumia zaidi ya wanafunzi 40, ikijumuisha bwalo la chakula, stoo, na jiko. 

Hosteli hii pia itahudumia wageni wanaokuja kwa makundi, hivyo kusaidia kukuza utalii ndani ya Hifadhi ya Ruaha,” alisema Meing’ataki.

Ongezeko la Watalii wa Ndani

Moja ya mafanikio makubwa yanayojivuniwa na uongozi wa hifadhi hiyo ni ongezeko la watalii wa ndani, hasa wanawake, ambalo linahusishwa moja kwa moja na juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuutangaza utalii wa Tanzania kupitia filamu ya The Royal Tour.

 Meing’ataki alieleza kuwa filamu hiyo imeamsha ari ya Watanzania kutembelea hifadhi za taifa, jambo ambalo halikuwepo hapo awali.

“Watalii wa ndani, hasa wanawake, wamekuwa wakiongezeka sana.

 Tunamshukuru Rais kwa juhudi zake, kwani mafanikio yake yameleta matokeo chanya, na hata kwetu hapa Ruaha tumeona ongezeko hilo,” aliongeza Meing’ataki.

Hifadhi ya Ruaha na Upekee Wake

Hifadhi ya Ruaha ni ya kipekee kwa ukubwa wake na wingi wa wanyama wakubwa kama tembo, simba, na nyati. Meing'ataki alibainisha kuwa hifadhi hiyo inatumia asilimia 30 tu ya eneo lake kwa shughuli za utalii, huku ikiwa na idadi kubwa ya tembo na simba, kiasi kwamba tafiti zinaonesha kuwa moja ya nane ya simba wote barani Afrika wanapatikana Ruaha.

“Hakuna hifadhi yoyote katika ukanda wa Afrika Mashariki yenye idadi kubwa ya tembo kama Ruaha. Vilevile, idadi ya simba ni kubwa, jambo linalofanya Ruaha kuwa kivutio cha kipekee,” alisema.

Uhusiano na Jamii Jirani

Maadhimisho ya miaka 60 ya Hifadhi ya Ruaha yamekuja na shukrani kwa jamii zinazozunguka hifadhi hiyo, ambazo zimekuwa sehemu muhimu katika uhifadhi na ulinzi wa mazingira. Meing'ataki alibainisha kuwa mahusiano bora kati ya hifadhi na jamii yamepelekea kupungua kwa matukio ya ujangili na uharibifu wa mazingira.


“Zamani, askari walikuwa wakipokea maelekezo ya kumkamata yeyote anayekutwa ndani ya hifadhi bila kibali. Lakini sasa, kupitia mawasiliano mazuri na viongozi wa vijiji, jamii imeelimishwa na kushirikishwa katika juhudi za kutunza hifadhi. Tumeshuhudia silaha za jadi zikiwa zinasalimishwa kwa hiari, jambo linalosaidia kupunguza ujangili,” alisema Meing’ataki.


Maendeleo ya Jamii Jirani

Aidha, uongozi wa hifadhi umekuwa ukitekeleza miradi mbalimbali ya kijamii kama kujenga shule, kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi, na kutoa mikopo ya kimaendeleo kwa wanawake. 

Miradi hii imekuwa chachu ya maendeleo kwa jamii inayozunguka hifadhi hiyo.

“Tunashirikiana na mradi wa Regrow kutoa misaada mbalimbali kwa jamii, ikiwemo ufadhili wa elimu kwa wanafunzi, kujenga shule na madarasa, pamoja na kuwawezesha wanawake kwa kuwapatia mikopo yenye riba nafuu ili waweze kujiajiri na kukuza biashara zao,” alifafanua Meing’ataki

Madhimisho ya miaka 60 ya Hifadhi ya Ruaha Kilele Chake kitakuwa jumatatu Oktoba 7 na Mgeni Rasmi ni waziri wa Maliasili na utalii Balozi Dkt Pindi Chana ikumbukwe kuwa maadhimisho haya yanadhihirisha mafanikio makubwa, si tu katika sekta ya utalii bali pia katika maendeleo ya jamii na uhifadhi wa wanyamapori.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI