NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Jumla ya madaktari sita na muuguzi mbobezi mmoja (Madaktari wa Rais Samia Suluhu Hassan) wamefika katika hospitali ya wilaya ya Mbeya Inyala kwa ajili ya kutoa huduma ya matibabu kwa wananchi hususani wa uchumi wa chini ambao wamekuwa wakihangaika kusafiri kwenda umbali mrefu kufuata huduma za kibingwa.
Madaktari hao wamepokelewa katika hospitali ya wilaya katika kata ya Inyala ambapo akizungumza kwenye hafla hiyo mkuu wa wilaya ya Mbeya Mhe. Beno Morris Malisa, ameelekeza shukrani zake kwa Serikali kuu chini ya Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa madaktari hao wa kada mbalimbali ili kuwafuata wananchi hadi ngazi za chini (wilayani).
Malisa amewataka wananchi kutumia fursa hiyo kuhamasishana kufika hospitali hapo ndani ya siku saba kupata matibabu juu ya maradhi yanayowakabili.
"Nitumie fursa hii kumshukuru sana Mhe.Rais, hii kazi yenu (madaktari) ni ya kujitolea kwahiyo naamini wananchi wetu watanufaika kwahiyo umati huu hamasishaneni ndugu, jamaa na marafiki waje ndani ya siku saba, Dkt. Samia ametuletea huduma hadi huku chini tunataka nini, gunia la chawa! Kwahiyo tunashukuru sana ", amesema Beno Malisa mkuu wa wilaya ya Mbeya.
Kwa upande wake mganga mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Mbeya Dr. Ahmad Suleiman, amesema wamewapokea madaktari hao kwa awamu ya pili ambapo ni pamoja na wale wa magonjwa ya akina mama na watoto, daktari wa upasuaji, daktari wa kinywa na meno na daktari wa ganzi na usingizi wakiwa wameambatana pia na muuguzi mbobezi.
Wananchi waliokuwa hospitalini hapo kwa ajili ya kupata matibabu wamesema wana imani na madaktari hao kuwa watasaidika na kuelekeza shukrani zao kwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa wataalam hao hadi wilayani kwa ajili ya kutoa huduma za kiafya badala ya kusafiri kwenda hospitali za rufaa na hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dar es Salaam.
0 Comments