Na Friday Simbaya, Mbeya
Safiri Luaga, mnufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) kutoka Kata ya Iziwa, Mbeya, ameweza kufanikiwa kuunda kikundi chenye wanachama 12, wakiwemo wanaume wawili na wanawake kumi, kupitia msaada wa TASAF.
"Kikundi chetu hukutana kila Jumatano, na tunachangia shilingi 1,000 kila mmoja. Tunakopesha shilingi 10,000 na kurudisha shilingi 10,500. Kutokana na mikopo hiyo, tumeweza kujenga uwezo wa kiuchumi na kuhudumia familia zetu. Hii yote ni kwa msaada wa TASAF," alisema Luaga.
Meneja wa Idara ya Kuweka Akiba na Kukuza Uchumi wa Kaya wa TASAF, Sarah Mshiu, alitoa shukrani kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua na kuunga mkono jitihada za TASAF za kuboresha maisha ya walengwa nchini.
Mshiu alieleza haya leo, Oktoba 26, 2024, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungwa kwa Maadhimisho ya Huduma za Fedha Kitaifa yaliyofanyika jijini Mbeya, viwanja vya Ruanda Nzovwe.
Amesema mpango wa TASAF unalenga kusaidia kaya maskini kwa kuwapatia fursa za kuweka akiba na kukuza uchumi kupitia miradi midogo midogo, ambayo inaongeza kipato na kuboresha hali ya maisha ya walengwa.
"Tunaichukulia Wiki ya Huduma za Fedha kama fursa muhimu ya kuwafikia walengwa wetu na kuwashirikisha katika shughuli za kifedha. Tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za TASAF za kutoa msaada wa kifedha na elimu kwa walengwa ili kuwawezesha kujimudu kiuchumi," alisema Mshiu.
Mshiu pia aliongeza kuwa TASAF imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia kaya maskini, na ushiriki wao katika maadhimisho hayo umewaletea tuzo za ushiriki na zawadi mbalimbali kwa kuonyesha mafanikio ya programu hiyo.
0 Comments