Na Thobias Mwanakatwe,Manyoni
MKOA wa Singida umetenga hekta 6000 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda ambapo kwa sasa mkoa una kiwanda kikubwa kimoja vya kati 10, vidogo 309 na vidogo kabisa vipo 1483.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, alimweleza hayo jana Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Jerry Silaa, ambaye yupo kwenye ziara ya siku tano mkoani hapa kukagua miradi ya maendeleo.
"Kumekuwa na mwamko wa kujenga viwanda katika Mkoa wa Singida, hivi sasa kuna viwanda vitatu vikubwa ambavyo vimejengwa na vitazinduliwa hivi karibuni ambavyo ni kiwanda cha mafuta ya kula ya alizeti, kiwanda cha Sabuni za mche na kiwanda cha juisi,"alisema Dendego.
Kuhusu umeme, alisema hivi sasa vijijji vyote 441 vya Mkoa wa Singida vimeshafikishiwa huduma ya umeme na hatua inayofuata umeme umeanza kupelekwa kwenye vitongoji lengo ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya umeme.
Aliongeza kuwa maendeleo makubwa yamefanyika katika mkoa huu kutokana na fedha nyingi kuletwa ambapo bajeti ya mwaka uliopita zilipangwa kuletwa Sh.bilioni 239 lakini zilizoletwa ni Sh.bilioni 241. kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Kuhusu madinj, alisema mkoa umefanikiwa kuongeza ukusanyaji wa mapato yanayotokana na madini kutoka Sh.bilioni 4.7 zilizokuwa zikikusanywa mwaka 2021 hadi kufikia Sh.bilioni 13.7.
Alisema uwekezaji katika sekta ya madini umeendelea kushika kasi katika mkoa huo ambapo wachimbaji wadogo na wakubwa wanaongezeka na hadi sasa leseni 821 za uchimbaji madini zimetolewa kwa wachimbaji.
Naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Silaa, alipongeza maendeleo makubwa yanayoonekana katika Mkoa wa Singida na kwamba ushirikiano baina ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali ni wa muhimu sana kwa kuwa ndio unasaidia kufanyika vizuri kwa shughuli za maendeleo.
Alisema kunapokuwa hakuna ushirikiano kati ya chama na serikali muda mwingi unatumika kwa ajili kutatua migogoro badala ya kuwahudumia wananchi.
"Kunapokuwa hakuna ushirikiano kunapokuwa migogoro,kunapokuwa hakuna kusemezana baina ya muuza duka na mwenye duka muda mwingi utatumika katika kutatua migogoro badala ya kuwahudumia wananchi," amesema.
MWISHO
0 Comments