MENEJA WA CHAMA KIKUU CHA USHIRIKA IRINGA (IFCU) TUMAIN LUPOLA
Na, Matukio daima App Iringa,
Chama kikuu cha ushirika mkoa wa Iringa, leo kimefanya mafunzo ya uongozi, utawala Bora na utunzaji wa kumbukumbu kwa viongozi wa vyama vya ushirika.
Meneja wa chama kikuu cha ushirika mkoa wa Iringa, Tumain Lupola, amesema lengo la mafunzo hayo, ni kuwajengea uwezo viongozi wa vyama vya msingi.
Akifungua mafunzo hayo, Lupola, amewataka viongozi wa Amcos kusimamia misingi ya uongozi bora hasa kanuni ya kurithishana uongozi kupitia mchakato wa uchaguzi ili kuwa ni viongozi wenye uwezo.
Amesema vyama vingi vinashindwa kukua kutokana na viongozi wake kuto kufanya vikao vya kikatiba na kuwashirikisha wanachama malengo ya chama kikuu, pamoja na kusikiliza changamoto zinazo wakabili.
Lupola ameongeza kuwa kutokufanya vikao kunasababisha vyama vingi kuendeshwa kwa mazoea jambo ambalo linapelekea kushindwa kutatuliwa kwa changamoto zilizojitokeza, namna ya kuzikabili changamoto mpya.
Katika hatua nyingine, amewataka wenyeviti kutambua uwezo wa wanachama wao ili kuwapa nafasi ya kuongoza pindi wanapopatwa dharura mbali mbali ikiwemo kusafiri pamoja na kuwaachia baadhi nafasi za mafunzo ili kuwaoongezea maarifa wanachama wao.
Aidha, Lupola amesema vyama vingi vya msingi vinakabiliwa na changamoto ya ukaguzi kutokana na kushindwa kuandika vyema kwenye vitabu vyao pamoja na kutokuwa na tabia ya kutoa risiti, jambo ambalo linafanya waonekana kuwa na matumizi mabaya.
"Kuna viongozi wanashindwa kuandika namba vizuri, mfano unakuta mtu ameuza mbolea ya shilingi milioni mia moja hamsini alafu kwenye kitabu anaandika milioni kumi na tano, hapo lazima upate hati chafu" alisema Lupola.
Hata hivyo, amesema chama kikuu cha ushirika kimekuwa kikijiendesha kwa hasara kutokana na viongozi wa viongozi wa vyama vya msingi, kushindwa kurudisha fedha za pembejeo kwa wakati, huku wengine wakipoteza kabisa fedha hizo.
Kwa upande wao viongozi walioshiriki mafunzo hayo, wamesema changamoto zinazowakabili ni ukosefu wa fedha kwa vyama vya msingi, hali inayopelekea kutoa ajira kwa watendaji wasio na uwezo wakutosha, huku wakiomba chama kikuu kuendelea kuwashika mkono ili kufikia malengo ya wakulima.
0 Comments