Na Fatma Ally Matukio DaimaApp, Dar
Chama Cha ACT Wazalendo kimeiomba Wizara ya TAMISEMI kuimarisha utaratibu wa mchakato wa uchaguzi baina yake na Halmashauri na wadau wa uchaguzi hasa vyama vya siasa ili kuondoa sintofaham ambayo imeanza kujitokeza kwa baadhi ya maeneo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ado Shaibu amesema hakuna mtiririko juu ya utoaji wa taarifa na maelekezo kuhusu utaratibu mzima wa Uchaguzi, kila ngazi na kila eneo wasimamizi au wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi huu wanatoa taarifa wajuavyo wao na kwa muda wanaoupanga wao.
Amesema kuwa, bado hawaoni jitihada za kutosha za utoaji wa taarifa na elimu kuhusu uchaguzi wa Serikali za mitaa hivyo wanatoa rai elimu itolewe kwa wakati na kwa kiwango kinachohitajika ili kila mtu awajibike kwa nafasi yake.
"Pamoja na kwamba TAMISEMI wametoa kanuni na mwongozo kuhusu mchakato mzima wa uchaguzi lakini katika zoezi la vyama vya siasa kutoa mawakala wa uandikishaji wa wapiga kura imeishia kuelezwa kuwa ni haki ya vyama kupeleka mawakala katika vituo vya kuandikisha wapiga kura tu."amesema Ado.
Ameongeza kuwa kuelekea siku ya kupiga kura ili kuondosha sintofahamu zilizojitokeza wakati wa maandalizi ya kuandikisha wapiga kura, TAMISEMI inapaswa kueleza ni lini najina ya mawakala yanapaswa yawe yamewasilishwa kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi na lini wataapishwa ili kuvipa vyama nafasi ya kujiandaa.
"Kwa Mujibu wa kanuni ya Uchaguzi na Kalenda ya Matukio, TAMISEMI wameonesha kuwa Fomu ya kuaomba kuteuliwa kuwa mgombea itachukuliwa siku zisizopungua ishirini na sita kabla ya siku ya Uchaguzi Kif. 17 (1) na kutakiwa kuzirejesha ndani ya siku saba Kif. 17 (2). Hii maana yake Fomu ya uteuzi itatolewa kwa siku moja tu yaani tarehe 1 Novemba, 2024 isipokuwa unaweza kurejesha wakati wowote ndani siku saba (tarehe 1 mpaka 7), wameshindwa kuzingatia kuwa upo uwezekano wa mgombea kuumwa au kupata tatizo litakalopelekea yeye kushindwa kwenda kuchukua Fomu siku hiyo" amesisitiza Ado.
Hata hivyo amesema TAMISEMI iweke utaratibu rafiki wa vituo vya kuapishia mawakala badala ya kuwataka mawakala hao wasafiri kwa umbali mrefu kufuata kuapishwa wakati hali halisi kinachofanyika kwenda kujaza fomu za kiapo jambo ambalo linaweza kufanyika mahala popote karibu yao bila kuathiri maana na mantiki ya kiapo hicho.
Sambamba na hayo amesema ACT Wazalendo watashiriki Uchaguzi wakipambana hivyo kuwasihi Wananchi kujitokeze kwa wingi kwenda kujiandikisha katika daftari la Wakaazi wa Mtaa ili watumie haki yao vizuri katika Uchaguzi huu kuwachagua wawakilishi wanaowaona kuwa wataweza kusimamia maendeleo ya maeneo yao.
0 Comments