NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi tarehe amehitimisha ziara ya kikazi kwa kutembelea Kata ya Uru Mashariki na kukagua miradi ya maendeleo katika shule za Sekondari Mnini na Mruwia, na shule za Msingi Kyaseni na Mruwia. pamoja na Kituo cha Afya cha Kyaseni.
Katika ziara hiyo, Mbunge aliambatana na Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini Ramadhani Mahanyu na Katibu wa Umoja wa Wanawake Wilaya Oliva Ngalawa na Diwani wa Kata ya Uru Mashariki Samweli Materu na Diwani wa viti maalumu Delina Temba.
Pia walikuwepo mwakikishi kutoka Ofisi ya mipango Halmashauri ya Moshi, uongozi wa CCM Kata ya Uru Mashariki na mtaalamu kutoka MUWSA na wataalamu kutoka Kata ya Uru Mashariki.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Materuni, Mbunge aliwaeleza wananchi kuwa katika kipindi cha Ubunge wake kwa miaka minne iliyopita, Kata hiyo imepokea kiasi cha shilingi bilioni 3,565,023,983.00. kutekeleza miradi ya maendeleo katika nyanja mbalimbali.
Miradi hiyo ni pamoja na kuanza kwa ujenzi wa barabara za Mamboleo Materuni na Mamboleo Shimbwe kwa kiwango cha lami huku miradi mingine mikubwa ni ile ya ujenzi wa daraja la RAU ambalo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alifika kuweka jiwe na Msingi, mradi wa maji katika kijiji cha Mnini na usambazaji wa umeme wa REA katika Kitongoji cha Wondo katika Kijiji cha Materuni.
Mbunge akiwa katika mkutano wa hadhara alielezwa kero mbalimbali zikiwemo zile za ubovu wa barabara za ndani, ujenzi unaosuasua wa barabara ya lami na ubovu wa mifereji ya asili katika Kata ya Uru Mashariki.
Kwa kuwa wawakilishi wa TARURA na TANROAD hawakuwa na mwakilishi katika mkutano huo kujibu kero zao, Mbunge alisema kuwa atazifikisha kwenye mamlaka husika huku kuhusiana na kero ya mifereji, Mbunge alisema kuwa yeye na Diwani wataendelea kutafuta wadau wa kusaidia kuijenga.
Wakiongea katika mkutano huo, Katibu wa CCM wilaya, Ramadhan Mahanyu na yule wa UWT, Oliva Ngalawa waliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao wakati wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la mkazi linalotarajiwa kuanza leo hadi Oktoba mwaka huu.
Walishauri wananchi wote washiriki kikamilifu kwenye uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa na kasema ni vyema wananchi wa Kata ya Uru Mashariki wakaendelea kuwaunga mkono viongozi wao kwani Serikali ya awamu ya sita, chini ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanya miradi mikubwa ya maendeleo katika Kata yao.
Mahanyu alikemea vikali tabia mbaya ya ulevi uliokithiri kwa baadhi ya vijana.
Mwisho.
0 Comments