BENKI ya NMB imetoa misaada ya Afya na Elimu kwa Zahanati tatu na Shule za Msingi mbili na Sekondari moja kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani vyenye thamani ya shilingi milioni 21.
Aidha misaada hiyo ni pamoja na madawati 100 na viti na meza 50 kwa Shule hizo, vitanda sita, viti vya kusubiria wagonjwa sita, vipimo sita vya kupimia shinikizo la damu na magodoro sita.
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nikson John akipokea vifaa hivyo kwenye Shule ya Sekondari ya Dk Samia Suluhu Hassan amesema kuwa benki hiyo imefanya jambo zuri kuisaidia serikali kupitia sekta ya afya na elimu.
John amesema kuwa miradi hiyo ni muhimu sana kwani wananchi bila ya kuwa na afya njema hawawezi kufanya shughuli zao.
Naye meneja wa Kanda Seka Urio amesema kuwa benki imekuwa ikitoa misaada kwenye sekta ya afya na elimu na kwa wananchi wanaokumbwa na majanga.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Regina Bieda amesema kuwa benki hiyo ni wadau muhimu katika suala la maendeleo ya wananchi.
Zahanati zilizopatiwa vifaa hivyo ni pamoja na Mpiji, Kipangege na Msufini huku Shule zikiwa ni Sekondari ya Dk Samia Suluhu Hassan, Shule za Msingi Muungano na Mtongani.
Mwisho.
0 Comments