Na Thobias Mwanakatwe,DODOMA
WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imelipongeza Shirika la Inades Formation Tanzania (IFTz) na Brooke East Africa na wadau wengine kutokana na kuwa mabingwa wa kuhakikisha mnyamakazi Punda hatoweki hapa nchini.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk.Edwin Mhede,ametoa pongezi hizo leo (Septemba 26, 2024) wakati akifungua warsha ya wadau ya uwasirishaji wa tathimini ya ustawi wa wanyama inayofanyia jijini Dodoma.
Amesema kiuchumi punda ni mnyama muhimu sana kwani anaingiza Sh.7000 kwa siku hivyo sio wa kumbeza na pia ana historia na ni sehemu ya ufahari kwa jamii kwani mtu anayekuwa na punda anaonekana anakuwa na viashiria vya kuwa mtawala.
Dk.Mhede amesema kwa kutambua umuhimu wa punda kiuchumi, serikali itaendelea kuchukua hatua za kudhibiti biashara haramu ya Punda nchini kwa uzito unaostahili kwa kuhakikisha anahifadhiwa na kulindwa ili mnyama huyo asiweze kutoweka hapa nchini.
Amesema wanaoebdelea na biashara ya punda watambue kwamba serikali haijalala itaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha mnyama kazi punda anastawi na ndio maana Oktoba Mosi 2022 ilisitisha shughuli za kuchinja punda na baishara ya ununuzi wa ngozi ya mnyama huyo.
"Serikali yetu chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inachukua hatua na itaendelea kuchukua suala hili kwa uzito unaostahili ili kuhakikisha punda wanahifadhiwa lakini pia kudhibiti biashara haramu inayowalenga punda," amesema Dk.Mhede.
Dk.Mhede ametoa wito kwa watu wanaokwenda kinyume na agizo la serikali kuwa wanakengeuka tu na sio jambo jema kwa taifa letu ambalo lina watu watiifu anbao wana ustarabu wa kutii sheria za nchi.
Awali Mkurugenzi wa Shirika la Inades FormationTanzania (IFTz), Mbarwa Kivuyo, amesema mradi wa kuboresha ustawi wa mnyama kazi punda ambao unatekelezwa katika mikoa ya Dodoma, Iringa na Singida umeanza kutekelezwa 2019.
Kivuyo amezema tangu umeanza kutekelezwa kumekuwa na matokeo chanya kwa kufanikisha kusitisha biashara ya punda ambayo ilishamiri sana hapa nchini kuanzia 2014 hadi 2022 hali iliyokuwa inahatarisha kupotea kwa mnyama huyo.
Katika warsha hiyo wadau walipokea taarifa ya hali ilivyo sasa baada ya katazo la serikali la kuzuia uchinjaji punda lililotolewa na serikali 2022, sheria ya ustawi wa punda na uboreshaji wa mitaala katika vyuo vya mifugo.
0 Comments