Header Ads Widget

WATAHINIWA 1,230,780 WAANZA MTIHANI KUMALIZA ELIMU YA MSINGI LEO

 



NA MATUKIODAIMA App, DAR

JUMLA ya watahiniwa 1,230,780 wameanza kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PSLE), huku Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) likiwatahadharisha kufuatia matokeo watakaobainika kufanya udanganyifu.

Tahadhari hiyo ilitolewa jana Septemba 10,2024 na Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Said Mohamed wakati akitangaza maandalizi ya mtihani huo kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, ambapo mtihani huo utafanyika kwa siku mbili kuanzia leo na kuhitimishwa kesho Septemba 12,2024.  

Mohamed alisema katika watahiniwa hao, 564,176 sawa na asilimia 45.84 ni wasichana na wavulana ni 666,604 sawa na asilimia 54.16.

Pia alisema watahiniwa wenye mahitaji maalumu waliosailiwa kufanya mtihani huo ni 4,583 kati yao 98 ni wasioona,1402 wenye uoni hafifu,1067 wenye uziwi, 486 wenye ulemavu wa akili na 1530 ni wenye ulemavu wa viungo.


“Kati ya watahiniwa 1,230,780 waliosajiliwa kufanya mtihani mwaka 2024, watahiniwa 1,158,862 sawa na asilimia 94.16 watafanya mtihani wa lugha ya Kiswahili na watahiniwa 71,918 sawa na asilimia 5.84 watafanya mtihani wa lugha ya kiingereza ambayo wamekuwa wakiitumia katika kujifunzia,”amesema katibu huyo.

Kuhusu masomo watakayotahiniwa, alisema ni sita ambayo ni Kiswahili, kiingereza, sayansi na teknolojia, hisabati, maarifa ya jamii, stadi za maisha na uraia.

Kuhusu maandalizi alisema yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa karatasi za mitihani na nyaraka zote muhimu zinazohusu mtihani huo kutoka halmashauri na manispaa zote nchini.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI