Header Ads Widget

TAWA YATAKA WANANCHI KUCHANGAMKIA FURSA KUANZISHA MASHAMBA YA WANYAMAPORI

 


Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA 


MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imetoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa kwa kuanzisha mashamba ya wanyamapori katika mikoa yao yenye hifadhi ili wajipatie kipato na hivyo kujikwamua na umaskini.


Afisa Mhifadhi Wanyamapori Kanda ya Kati, Ogossy Gasaya, ametoa wito huo leo (Septemba 11, 2024) kwenye maonesho ya saba ya kitaifa ya Mifuko ya Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yanayofanyika kitaifa mjini Singida.



Amesema wamekuja kutoa elimu kwasababu wananchi wengi bado hawajui kama kuna fursa za kiuchumi zilizopo Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia taasisi ya TAWA.


Gasaya amesema miongoni mwa fursa zinazopatikana ni pamoja na uanzishaji wa mashamba ya ufugaji wanyamapori,uanzishaji mabucha ya kuuza nyamapori na uanzishaji wa 'zoo' .



Amesema katika fursa ya uanzishaji mashamba ya wanyamapori yaliyopo na mikoa yao,wananchi wanaweza kutengeneza ratiba maalum ya kutembelea maeneo hayo na hivyo kujipatia pesa.


"Wananchi wakichangamkia fursa ya kuanzisha mashamba ya wanyamapori, TAWA inatoa mbegu na muongozo wa namna ya kuyaanzisha hayo mashamba ambapo miongozo yote inapatikana katika ofisi za TAWA zilizopo kwenye kanda zote," amesema.



Gasaya amesema kwa upande wa uhifadhi,TAWA haipendi  kuona wananchi wanalipiza kisasi kwa kuwaua wanyama pori wanapoharibu mazao yao hivyo imekuwa ikitoa elimu ili waendelee kuwa rafiki wa wanyamapori na kutoa taarifa kwa mamlaka zinazohusika kunapotokea uharibifu umefanywa na wanayama.


Ameongeza kuwa TAWA imekuwa ikitoa Dola za Kimarekani 5000 kila mwaka zinazotokana na uwindaji wa kitalii kwa vijiji vinavyopakana na hifadhi ili waendelee kuona umuhimu wa uhifadhi na kutoa ushirikiano.



Amesema pia asilimia 25 ya makusanyo ya jumla ya shughuli za utalii inayotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa vijiji vinavyopakana na mapori ya uhifadhi ambayo inatolewa kwa misimu miwili.


Naye Afisa Wanyamapori msaidizi kanda ya kati, Kanunga Marau, amesema TAWA kwa kutambua umuhimu wa uchumi wa wananchi imekuwa ikitoa elimu kuhusu wanyamapori waharibifu na wakali.


MWISHO

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI