Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA
MKUU wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, amesema uuzaji mazao kwa kutumia mfumo wa stakabadhi za Maghala umeleta mapinduzi makubwa katika biashara ya mazao mkoani hapo ambapo bei ya Dengu imepanda hadi kufikia Sh.2060 kwa kilo.
Akizungumza leo (Septemba 6, 2024) na waandishi wa habari kutoa ufafanunuzi kuhusu mfumo wa shakabadhi ghalani amesema utaratibu huo umepunguza changamoto zilizokuwa zinawakumba wakulima kama vile upotevu wa mazao,bei duni na unyonyaji kutoka kwa wafanyabiashara.
"Kumekuwa na ongezeko la bei ya zao la dengu ambapo ilikuwa ikiuzwa kati ya Sh.900 hadi 1300 kwa kilo katika msimu wa 2023/2024 na sasa inauzwa kati ya Sh 1,670 hadi 2,060 kwa kilo kwa msimu wa 2024/202/," amesema Dendego.
Dendego amesema kutokana na mafakikio hayo serikali ya Mkoa wa Singida itaendelea kuhamasisha wakulima kutumia mfumo wa wa stakabadhi ghalani kwa faida ya maendeleo ya kilimo na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Amesema pamoja na mafanikio katika kutumia mfumo huo kumekuwa na changamoto kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kutokubaliana na mfumo huo kwa madai hawapati faida kubwa ambayo walikuwa wanapata awali kwasababu ya kununua mazao kwa wakulima kwa bei ndogo na kutumia vipimo visivyo sahihi.
Amesema kutokana na kuongezeka kwa bei ya Dengu kumeongeza mapato katika halmashauri,kumedhibiti utoroshaji wa mazao,kufanya serikali kuwa na uhakika wa takwimu,utengenezaji wa urahisi wa mikopo kwa wakulima na kuongezeka kwa masoko ya uhakika ya ndani na nje ya nchi.
Mkoa wa Singida ilizindua rasmi utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi ghalani kwa msimu 2024/2025 kufuatia maagizo yaliyotolewa na serikali kupitia mwongozo wa biashara ya zao la dengu,mbaazi na ufuta.
Mwongozo huo ulitolewa chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA),Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC),Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) na Soko la Bidhaa (TMX).
0 Comments