Na Fadhili Abdallah,Kigoma
POLISI mkoa Kigoma imemtia mbaroni mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Ramadhani Shaban (21) Mkazi wa Buronge Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kwamba ametekwa ili kuwezesha ndugu zake kutoa fedha kwa watekaji aweze kukombolewa.
Kamanda wa polisi mkoa Kigoma, Filemon Makungu alieleza hayo akito taarifa kwa waandishi wa Habari mjini Kigoma alibainisha kuwa mtu huyo alitoa taarifa za uongo kwa wazazi wake (alijiteka) nia ikiwa kujipatia fedha.
Sambamba na mtuhumiwa huyo polisi pia inawashikilia watu wawili Kassimu Kibona na Ramadhani Issa ambapo mtu huyo alitoa taarifa kwa wazazi wake akidai ametekwa na watu wasiojulikana wanaodai kiasi cha shilingi milioni 2.5 ili waweze kumkomboa.
Akiwa mafichoni mtu huyo alikuwa akipiga simu kwa wazazi wake watoe fedha haraka ili waweze kumuachia kwani wakichelewa watekaji wanaweza kumuua ambapo
Kufuatia shinikizo hilo wazazi wa mtu huyo walitoa taarifa polisi ambapo upelelezi ulianza mara moja huku polisi wakiwasihi wazazi wa mtu huyo kutotuma fedha kwa mtu yeyote kuhusiana na tukio.
Kamanda huyo wa polisi mkoa Kigoma alisema kuwa wakati polisi wakiendelea na upelelezi Ramadhani alifikishwa na wazazi wake kituo kikuu cha polisi mkoa Kigoma wakieleza kuwa amepatikana eneo la Msimba Dampo nje kidogo ya manispaa ya Kigoma Ujiji baada ya kutoa fedha kwa watekaji.
Polisi imeeleza kuwa uchunguzi wa kina walioufanya umegundua kuwa watuhumiwa walitoa taarifa za uongo kwa nia ya kujipatia fedha na hivyo kuwatia mbaroni ambapo wanatarajia kufikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika.
0 Comments