NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Mbunge wa Mbeya vijijini Mhe. Oran Manasse Njeza, amewataka wanafunzi kuendelea kusoma kwa bidii huku Serikali ikiendelea kuboresha miundombinu ya kielimu katika jimbo lake ili kuhakikisha wanafikia ndoto zao akiahidi kwa atakayepata wastani wa A kununua kwa shilingi laki moja kote jimboni kwake.
Njeza ametoa ahadi hiyo wakati akipata chakula cha mchana pamoja na wanafunzi wa shule ya msingi Mwela kata ya Ilungu, ikiwa ni kwenye mwendelezo wa ziara yake akikutana na wananchi wake na kusikiliza kero zinazowakabili na kutembelea miradi na shule mbalimbali.
Baada ya kufika shuleni hapo (S/msingi Mwela), ameeleza kufurahishwa na shule zilizoshirikiana na wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanapata chakula shuleni na kuwashukuru wananchi kwa kuzingatia umuhimu wa elimu ambao imekuwa himizo lake kubwa.
Mbunge huyo wa jimbo la Mbeya vijijini amechangia shilingi laki mbili ili kuunga mkono kampeni hiyo ya chakula shuleni na kuitaka Serikali ya Halmashauri ya Mbeya kuunga mkono juhudi za wananchi na ofisi ya Mbunge kwa kuendelea kujenga na kuboresha miundombinu ya shule ya msingi Mwela kata ya Ilungu ili kuinua kiwango cha elimu katani humo.
Pia Mhe. Njeza amesema kwa watoto wote watakaopata wastani wa A kwenye matokeo ya darasa la saba (mtihani wa Taifa) atanunua ufaulu huo kwa shilingi laki moja.
Amesema elimu ni suala la kuzingatiwa na kupewa kipaumbele kwani Dunia ya sasa na baadaye ni ya kisomi zaidi hivyo bila elimu hakutakuwa na msaada.
"Ndugu zangu asiwadanganye mtu, elimu ndio utajiri wa kwanza, hapa nikiuliza mtu mwenye ekari 20 au 10 za mashamba si ajabu hakuna labda ekari tano wengi ni eka mbili au moja kwahiyo urithi pekee wa mtoto ni elimu kwasababu mashamba hamna kitu. Endeleeni kutoa chakula kwa watoto wetu na mimi ninawakabidhi laki mbili ili kununua walau maharage watoto wale chakula kizuri shuleni kwetu", amesema mbunge Njeza wakati akizungumza na wananchi na wanafunzi wa kijiji cha Mwela kata ya Ilungu Mbeya vijijini..
0 Comments