NA WILLIUM PAUL, SAME
MBUNGE wa Jimbo la Same mashariki wilayani Same mkoa Kilimanjaro, Anne Kilango Malecela ameitaka Wakala wa Barabara vijijini na mjini (Tarura) kuhakikisha anazifungua Barabara za kata ya Bwambo ili kufungua uchumi wa kata hiyo.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mbunge huyo kufanya mkutano wa hadhara na wananchi hao jana ambapo walilalamikia ubovu wa Barabara ya Saweni - Gavao- Bwambo ambayo ndio Barabara muhimu kwao.
Mbunge Anne alisema kuwa, barabara ndio inayoleta maendeleo lakini kwa sasa kata ya Bwambo maendeleo yamesimama kutoka na ubovu wa Barabara.
"Kata ya Bwambo ni lazima ifunguke kwa kufua barabara vijana waweze kufanya shughuli zao sasa hili ni jukumu la Tarura niwaombe sana tusaidieni kufungua hizi barabara zetu za kata ya Bwambo" Alisema Anne.
Akijibu kero hiyo ya barabara, Meneja wa Tarura wilaya ya Same, Mhandisi James Mnene alisema kuwa, barabara ya Saweni- Gavao - Bwambo yenye urefu wa kilomita 25 ipo kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha na Mkandarasi wake ameshapatika muda wowote ataingia saiti.
"Hii barabara ya Saweni - Gavao - Bwambo barabara hii ni korofi sana tumekuwa tukiitengea fedha kila mwaka na mwaka huu tumeshaipatia Mkandarasi ambapo anatarajiwa kuanza kazi mapema lengo ni kuhakikisha inapitika muda wote" Alisema Mhandisi Mnene.
Mhandisi huyo alisema kuwa, Tarura wilaya ya Same ilikuwa ikipokea milioni 660 kwa mwaka kama bajeti ya matengenezo ya barabara kwa majimbo mawili ya Same mashariki na same magharibi lakini toka kuingia kwa serikali ya awamu ya sita bajeti imeongezeka na kufikia Bilioni 6.7.
Aidha Mhandisi huyo alisema kuwa, ipo barabara ya Mamba - Mpinji - Bwambo - Vunta - Hedaru yenye urefu wa kilomita 42 ambapo kwa sasa wametenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kilomita 40.
Mwisho.
0 Comments