Header Ads Widget

MAWAKALA WA UTALII WAHOFIA MAPATO KUSHUKA

 


MWANDISHI WETU, KILIMANJARO

Mawakala wa Utalii mkoani Kilimanjaro, wameitaka serikali kuifuta mara moja Taasisi isiyo ya kiserikali iitwayo Kilimanjaro Porters Assitance Project (KPAP) kwa kile wanachodai taasisi hiyo inachafua taswira ya biashara ya utalii nchini.

Wanadai kuwa, KPAP inaeneza propaganda chafu za kuwachafua mawakala kuwa si waaminifu na wasiotoa huduma nzuri kwa wapagazi, jambo ambalo walidai si la kweli.

KPAP kupitia wavuti yake imetoa orodha ya makampuni ya wakala wa Utalii 45 ili kuiaminisha dunia kuwa hazo ndiyo kampuni zinazotoa huduma nzuri kwa wageni na wapagazi.

Mawakala hawa wanadia Taasisi hiyo imekuwa chanzo cha wao kukosa wageni mara kwa mara na kuweka rehani biashara ya utalii ambayo serikali ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imepambana kuutangaza duniani kwa gharama kubwa kupitia Filamu ya Royal Tour.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi wa Matata Tours, Matata Omari, alisema kinachofanywa na taasisi hiyo ni kuwaharibia biashara ya utalii ambayo wamekuwa wakilipa kodi kwa serikali na kutoa ajira kwa mamia ya wapagazi pamoja na waongoza watalii.

Kutokana na kadhia hiyo, Matata aameiomba serikali kupitia upya usajili wa Taasisi hiyo ikiwamo kuitisha katiba yake kuona kama kinachofanywa ni sahihi kwa mujibu wa katiba yake na kama hakiendani na katiba basi taasisi hiyo ifutwe mara moja.

"Hii ni project (mradi), huwezi ukalazimisha watu wawe members (wanachama) wako na akumbuke kujiunga na chama ni suala la hiari, kitendo cha kuwaambia wageni wasitumie kampuni ambazo si wanachama wa KPAP ni kinyume cha sheria na hii haikubaliki",alisema Mkurugenzi huyo.

Aidha Omari alisema hali hiyo imewaweka kwenye wakati mgumu mawakala kwani mara kwa mara wamekuwa wakiulizwa na watalii kama ni wanachama wa KPAP.

Nyaraka za mawasiliano baina ya wageni na mawakala zinaonyesha kuwa kama wakala hayupo kwenye Taasisi hiyo baadhi ya watalii wamekuwa wakifuta safari na kutafuta wakala ambaye ni mwanachama wa KPAP jambo ambalo alisema linawaweka kwenye mazingira magumu katika biashara hiyo ya utalii.

Wakala mwingine ambaye (jina lake tunalo), alidai kuwa katika siku za karibuni amepoteza wageni 10 kutokana na kutokuwa mwanachama wa KPAP na kusanbabisha ajira za watu 45 kupotea ambao ni pampja na waongoza wageni, wapishi, wahudumu na wapagazi 30 ambao pia wamekosa mishahara.

"Mbali na hilo Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) imekosa mapato kwa wastani wa Dola za Marekani 8,350 ikiwa ni park fees (viingilio) vya kupanda mlima Kilimanjaro.

"Hiyo ni trip moja ya wageni, jiulize kama kila mgeni atakataa kupanda mlima na kampuni ambayo haipo KPAP unatarajia nini kama si biashara ya utalii kuhodhiwa na watu wachache?,alihoji wakala huyo.

Wanaitaka serikali kuchukua hatua za haraka kuifuta KPAP ili kunusuru sekta ya utalii kwani mamia ya mawakala wa Utalii watafunga ofisi zao na marefu ya watu wanaotegemea ajira kupitia sekta ya utalii wataishia kuwa ombaomba huku serikali kwa upande wake ikikosa mabilioni ya fedha zinazotokana na tozo mbali mbali kupitia Utalii.

Meneja wa KPAP, Kelvin Salla alisema mawakala wanaopiga kelele juu ya mpango wao ni wale ambao hawalipi vizuri mishahara ya wapagazi kama ilivyoanishwa na Wizara ya Maliasili na Utalii ikiwa ni pamoja na kuwapatia milo mitatu pamoja na mavazi ya kujikinga na baridi. Alisema mawakala wanaofanyakazi na KPAP ni wale wanaofuata taratibu zote ikiwamo malipo ya mishahaa ya wapagazi, mavazi ya kujikinga na baridi.

Uongozi wa Hifadi ya Taifa ya Kilimanjaro (KINAPA) limeanza kushughulikia malalamiko hayo ikiwa ni pamoja na kukusanya taarifa sahihi.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu ameulizwa juu ya KPAP kujipa mamlaka ya kuwachagulia wageni mawakala wa kufanya nao kazi ambapo alidai amempa jukumu hilo Katibu tawala Mkoa wa Kilimanjaro.

"Hiyo taarifa nimeiona kwa RAS sijui kama amekamilisha maana alikuwa safari ndiyo amerudi leo,"alisema.

Alipotafuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Pindi Chana aliomba atafutwe baadaye na alipotafutwa tena simu yake iliita bila majibu.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI