Na Matukio Daima App
MAKAMU Mwenyekiti wa Umoja wa Wamachinga Tanzania,Steven Lusinde amesema kuwa Wafanyabiashara wadogo wadogo alimaarufu Wamachinga sio maadui wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) bali wao ni miongoni mwa chanzo kikubwa cha kuingiza mapato ya nchini.
Pia amehaidi kuwa umoja huo utakuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha elimu ya mlipa kodi inawafikia wafanyabiashara wote wakiwemo wa tabaka la chini hadi wafanyabiashara wakubwa.
Ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam katika kikao cha ndani kati ya Umoja huo na Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda wakati wakijadili mambo mbalimbali yanayowahusu katika biashara zao.
Alisema Umoja huo na TRA sio maadui kwani wao wanajamii kubwa inayojishughulisha na biashara hivyo hakuna Mfanyabiashara mkubwa pasipo kuwa na mfanyabiashara mdogo (Wamachinga) maana wao ndio wanauza bidhaa za hao wafanyabiashara wakubwa kwa mfumo wa rejareja.
"Bila sisi mfanyabiashara mkubwa hawezi fanyabiashara ,kwani sisi ndio tunaouzs kwa mfumo wa rejareja na tupo wengi mfumo huu,"alisema.
Alisema watahakikisha wanakuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wafanyakazi wa TRA wanafanya kazi zao katika mazingira mazuri ya ushirikiano kwani wao wanapaswa kupita kwenye masoko mbalimbali nchini kuelimisha wafanyabiashara wadogo wadogo faida za ulipaji wa kodi katika kukuza uchumi wa nchi na kuleta tija kwa kizazi kijacho.
"Sisi na TRA ni kitu Kimoja kwani mamlaka hii ipo ndani ya Tanzania na sisi ni wananchi wa Tanzania, tukipatiwa ushirikiano mkubwa kutoka kwa maafisa wa TRA kuanzia ngazi za kanda mpaka taifa, tunaamini tutafika pazuri katika kumsaidia Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa ujumla katika kukusanya mapato kwa njia ya kodi na tozo katika kuendelea kulijenga Taifa letu,"alisema na kuongeza
"Wamachinga hawana shida na TRA hata kidogo sasa ni wakati wa kujenga ushirikiano wa karibu katika kuhakikisha na sisi tunapewa ushirikiano katika hatua mbalimbali ikiwemo suala la elimu ya Mlipa kodi ili na sisi tujitoe katika kujenga taifa letu,"alisisitiza Lusinde.
Kwa Upande wake Kamishna Mkuu wa TRA ,Mwenda aliushukuru umoja huo kufika na kufanya mazungumzo naye na kuhaidi kutoa ushirikiano mkubwa katika usambazaji wa elimu ya mlipa kodi kupitia viongozi hao wakuu wa Machinga.
Miongoni mwa viongozi wa Juu wa Umoja huo waliokutana na Kamishna huyo ni pamoja na Mshauri wa Umoja wa Machinga,Shabani Matwebe,Mwenyekiti wa Kawasso,Stephen Lusinde pamoja na Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Dar es Salaam Namoto Yusuph.
0 Comments