Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA
WAKATI matukio ya watu kupotea na utekaji yakiripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini, wakazi wa kijiji cha Pugizi wilayani Ikungi mkoani hapa wametinga katika kituo cha polisi kuliomba Jeshi la Polisi liwasaidie kumtafuta ndugu yao aliyepotea katika mazingira ya kutatanisha zaidi ya miaka 30 iliyopita.
Wananchi hao ambao ni ndugu wa Asha Salum Nzile aliyepotea, walifika katika kituo cha polisi Singida mjini na kufungua faili PHQ/SIN/IRA/7004/2024 la kupotelewa na ndugu yao aliyepotea katika mazingira ya kutatanisha 1992 katika kijiji cha Pugizi,kata ya Mwaru Tarafa ya Sepuka Wilaya ya Ikungi.
Mtoto wa mwanamke huyo aliyepotea, Salum Rajab Nzile, alisema tangu mama yake alipotea wamefanya jitihada kadhaa za kumtafuta bila mafanikio ambapo kwa mara mwisho walipomuuliza mjomba yao aitwaye Jumanne Salum alidai Asha (aliyepotea) amempeleka mkoani Tabora.
Alisema baada ya kuelezwa hivyo na mjomba yake alikwenda hadi Tabora kumtafuta bila mafanikio na baadaye mwaka huu (2024) walifanya kikao cha familia kujadili aliko Asha.
Salum alisema katika kikao hicho mjomba yake alikiri kusema uwongo kwamba Asha yupo Tabora na baadaye alikubali kutoa mali zilizoachwa na mwanamke huyo aliyepotea ambazo ni ng'ombe 10 na ekari 10 za shamba ambavyo alivitoa Mei 2024.
Alisema makabidhiano ya mali hizo yalifanyika kwa kuandikishana katika ofisi ya kijiji chini ya usimamizi wa Mtendaji wa Kijiji na Mwenyekiti wa kijiji.
Hata hivyo, alisema katika hali ya kushangaza taarifa ya makabidhiano ya mali hizo ambayo yaliandikwa kwa maandishi kama ushahidi yamepotea katika mazingira ya kutatanisha kabla hajapewa nakala katika ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha Pugizi.
Aliongeza kuwa kupotea kwa taarifa hiyo kunamtia wasiwasi kwamba huenda kuna mchezo mchafu unataka kufanyika aje anyang'anywe mali hizo hivyo akaamua kulifikisha suala hilo kwa Mtendaji wa Kata ambaye alimuru iandikwe taarifa nyingine lakini hadi sasa hakuna utekelezaji.
Naye Rajabu Mrisho maarufu Kayanda ambaye mwanamke aliyepotea ni dada yake alisema kimsingi wamechoka kumtafuta ndugu yao hivyo wanaliomba Jeshi la Polisi liwasaidie kumtafuta.
Kayanda alisema wanandugu wanachotaka kufahamu ni kama mwanamke huyo yupo hai au ameshafariki kwani tangu alipopotea wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu sana kimaisha.
Naye Mahona Himu ambaye ni jirani na mwanamke huyo aliyepotea alisema wana imani kubwa na Jeshi la Polisi kwamba litafanya uchunguzi wa kina suala la kupotea kwa mwanamke huyo ili ukweli ukojulikana ndugu watakuwa na amani.
0 Comments