Mkuu wa mkoa wa Mbeya Juma Zubery Homera
NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Halmashauri ya Chunya mkoani Mbeya imemkabidhi mkandarasi kazi ya kuanza ujenzi wa kituo cha mabasi wilaya ya Chunya ili kuwaondolea adha wasafiri na kuinua hadhi ya wilaya hiyo.
Akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini ujenzi huo, mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Chunya Tamimu Kambona, amesema kukabidhiwa mradi kwa mkandarasi na kuanza ujenzi ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alipopita wilayani Chunya ikiwa ni maombi ya wananchi wakati wa ziara hiyo.
Kambona amesema Halmashauri ya Chunya inatumia mapato ya ndani kujenga stendi hiyo.
"Mheshimiwa mkuu wa mkoa stendi yetu ya Chunya tunaijenga kwa mapato yetu ya ndani kwa gharama ya shilingi Billion tatu ikiwa ni maelekezo ya Mhe.Rais (Samia Suluhu Hassan) na muda wa utekelezaji wa mradi ni miezi tisa na tunaamini mkandarasi atafanya kazi hii kwa wakati", ameeleza Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Chunya.
Serikali ya wilaya ya Chunya imeahidi kuhakikisha inasimamia ujenzi wa stendi hiyo usiku na mchana kuhakikisha mradi unakamilika kwa muda usiozidi miezi tisa ya mkataba.
Mkuu wa mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Zubery Homera, amemtaka mkandarasi kufanya kazi hiyo kwa ubora, wakati na uadilifu."Nitoe wito kwa taasisi zote TANESCO, watu wa Maji na wengine hakikisheni huduma hazikosekani hapa ili mkandarasi afanye kazi na stendi hii ikamilike kwa wakati. Chunya tunaenda vizuri madude yanaendelea kujengwa jengo la Halmashauri limejengwa, hapa tunashusha dude lingine (Stendi mpya Chunya) na madude mengine huko yanaendelea yote haya ni kwasababu Chunya mlichagua vizuri na msije mkachagua viongozi wa hovyo, viongozi wa hovyo si mnawafahamu!", amesema Homera.
Pia, Mkuu wa mkoa, ameitaka Serikali ya wilaya ya Chunya kuendelea kuwa karibu na mkandarasi na kusimamia ujenzi huo ili ukamilike kwa wakati na kuleta manufaa kwa wasafiri na wananchi kwa ujumla pamoja na Serikali kwa ujumla.
0 Comments