Jusline Marco;Babati.
Jumla ya timu 35 zinatarajiwa kushiriki michuano ya Chem chem CUP mwaka 2024 ambapo kiasi cha shilingi milioni 78 zinatarajiwa kutumika.
Michuano hiyo ya 10 kufanyika imezinduliwa na Mkuu wa mkoa Manyara,Queen Sendiga ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa wilaya ya Mbulu, Veronica Kessy .
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa michuano hiyo mwaka 2024, Kessy alipongeza Taasisi ya Chem Chem ambayo imewekeza wilayani Babati katika shughuli na Utalii na Uhifadhi kuendeleza michezo kupitia uhifadhi mkoani Manyara.
"Tunawapongeza Chem Chem kwa kuendeleza michuano hii kila mwaka ambayo inalenga kuendeleza uhifadhi wa mazingira na kupiga vita vitendo vya ujangili"alisema
Alisema serikali inadhamini mchango wa Chem Chem katika kuendeleza uhifadhi na kuwataka wananchi wa wilaya ya Babati kuendelea kushiriki katika uhifadhi kwani zipo faida kubwa zinazopatikana.
Naye Meneja Mkuu wa Chem Chem, Clever Zulu alisema Chem Chem itaendelea kudhamini michezo hiyo ili kuongeza uewelewa katika masuala ya uhifadhi,huku kauli mbiu ya mwaka huu ya michuano hiyo ni "Tunza Mazingira Okoa Twiga" ambapo mamia ya wakazi wanaoishi katika vijiji 10 ambavyo vinaundwa hifadhi ya jamii ya wanyamapori Burunge wanatarajiwa kushiriki.
Katibu wa michuano hiyo John Bura alisema katika timu 35 zitakazo shiriki michuano hiyo,kati ya hizo timu 18 ni timu za wakubwa za soka, timu 9 za vijana chini ya miaka 18 na timu 8 za wanawawake.
Kwa upande wake Afisa wanyamapori wilaya ya Babati, Christopher Laizer alisema lengo la michuano hiyo ni kuhamasisha utunzwaji mazingira,kutoa elimu juu ya uhifadhi,kupiga vita ujangili, kujenga mahusianno katika Jamii na kuimarisha afya za wadau.
0 Comments