Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu sera na uratibu wa bunge Wiliam Vangimembe Lukuvi akipa maelezo kwenye Banda la TAKUKURU
Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego akiwa na Waziri Lukuvi na viongozi wengine wakisoma vipeperushi
Na Thobias Mwanakatwe, Singida
TAASISI ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa Nchini (TAKUKURU) imeshiriki maonesho ya kitaifa ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yanayofanyika mkoani Singida.
Katika maonesho hayo ambayo yameanza Septemba 9, 2024 wananchi wameanza kumiminika katika banda la TAKUKURU kwa ajili ya kupata elimu ya rushwa hususani katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024 na uchaguzi mkuu utakaofanyika 2025.
Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Petro Horombe, akitoa maelezo leo (Septemba 10, 2024) kwa mgeni rasmi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge na Uratibu,William Lukuvi, amesema TAKUKURU imeshiriki maonesho hayo ili kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi ili waweze kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa.
Amesema TAKUKURU inatoa elimu hiyo katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajia kufanyika Novemba mwaka huu na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika 2025 kwani wananchi ni nguzo muhimu katika kuzuia vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi.
Horombe amesema wananchi wakijiepusha katika vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi nchi yetu itakuwa na uchaguzi mzuri usiokuwa na rushwa jambo ambapo linawezekana kabisa.
Amesema hivi karibuni TAKUKURU iliendesha mafunzo kwa ajili ya kuhamasisha jamii kujiepusha na vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi ambayo ilifanyika Julai 31, 2024 katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambapo washiriki walikuwa ni viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini na viongozi wa asasi za kirai.
Ameongeza kuwa katika mafunzo hayo kuliwekwa azimio la pamoja la kushirikiana katika kuhamasisha jamii ishiriki katika kudhibiti na kuzuia vitendo vya rushwa hususani katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.
Horombe amesema katika dhana ya mapambano dhidi ya rushwa kila mtendaji wa kata na kijiji kwenye eneo lake ndio kamanda namba moja katika mapambano dhidi ya rushwa.
Amesema Mtendaji wa Kata ni mlinzi wa amani katika eneo lake ambapo rushwa ni uharifu na ni kosa la jinai hivyo watendaji wanao wajibu wa kukomesha vitendo vya rushwa kwenye maeneo yao.
"Mfano kuna miradi inasuasua kata ya Isuna pengine kuna harufu ya rushwa Mtendaji anatakiwa kutoa taarifa TAKUKURU," amesema.
Amesema watendaji waliopo ndani ya serikali hawatakiwi kulalamika badala yake kila mtumishi achukue hatua za kuzuia rushwa kwenye eneo lake analolitawala.
Amesema wananchi wanapoelimika na kuhamasika kuichukia rushwa, kuikemea, kuikataa na kutoa taarifa vitendo vya rushwa TAKUKURU vitendo vya rushwa nchini vitaondoka kabisa.
Maonesho hayo yanatarajia kufungwa na Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa Septemba 14, 2024.
0 Comments