NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Mbarali kimetoa mafunzo kwa viongozi wake wa mataw, vijiji, kata pamoja na watia nia wa nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji katika Tarafa ya Ilongo.
Akizungumzia mafunzo hayo mwenyekiti wa CHADEMA jimbo la Mbarali Peter Mwashiti, amesema lengo ni kuwangenga viongozi na wagombea wa nafasi mbalimbali kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji.
"Ndugu zangu twendeni kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa na tukashinde, mwaka huu hakuna mtu kupita bila kupingwa. Namshukuru Libe Mwang'ombe (mtia nia ya ubunge jimbo la Mbarali) kwa kuwa tumekuwa tunashauriana mambo mengi hata hii semina au mafunzo haya ametuwezesha yeye kuhakikisha viongozi na watia nia wetu wanajifunza na kwenda kushinda", amesema Mwashiti.
Kiongozi huyo amewataka viongozi wa kata mbalimbali katika Tarafa hiyo na jimbo kwa ujumla kuhakikisha wanasimamisha wagombea kila eneo la uchaguzi ili wananchi kupata viongozi bora.
Kwa upande wake aliyekuwa mgombea ubunge jimbo la Mbarali Liberatus Mwang'ombe amesema ikiwa atahitajika na wananchi atagombea tena ubunge kwa ridhaa ya Chama chake (CHADEMA) akisema hajakata tamaa ya kuwatumikia wananchi.
"Nisiseme mengi, ila naomba tushikamane kuhakikisha uchaguzi huu tunashinda Serikali za vitongoji na vijiji kwamaana uchaguzi huu ni muhimu sana na ndio taswira ya uchaguzi mkuu wa mwakani", ameeleza Mwang'ombe.
Wakufunzi wa mafunzo hayo maalum kwa wagombea walikuwa ni aliyekuwa Katibu wa CHADEMA mkoa wa Mbeya George Titho pamoja na Emily Mwakilembe ambaye alikuwa katibu wa Baraza la vijana wa Chadema (BAVICHA) mkoa wa Mbeya.
Wawili hao kwa nyakati tofauti wamewataka viongozi na wagombea kujiamini na kusimama kwa dhati ili kwenda kuwatumikia wananchi kwa madai kuwa viongozi waliopita bila kupingwa uchaguzi uliopita wameshindwa kazi ikiwemo kutosoma mapato na matumizi na kushindwa kusimamia mwongozo wa chakula shuleni kwa watoto.
0 Comments