Header Ads Widget

TAKUKURU YAOKOA SHILINGI MILIONI 31 HALMASHAURI YA MJI TUNDUMA ZILIZOKOPESHWA KWA VIKUNDI MFU

Na Moses Ng'wat, Songwe.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Songwe  imeokoa zaidi ya Shilingi milioni  31,446,000 fedha za matumizi ya asilimia 10 za mapato ya ndani katika Halmashauri ya Mji Tunduma.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 23,2024, kwa lengo la kutoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Songwe, Frida Wikesi, amesema ufatiliaji uliofanyika juni mosi hadi 30, 2024  Takukuru ilifanikiwa kuokoa kiasi hicho cha fedha.

Wikesi amesema katika kipindi cha mwezi mmoja kuanzia Juni  Mosi hadi 30,   2024 Takukuru imeweza kukusanya kiasi cha shilingi 31,446,000 kutoka katika  makundi maalumu 20 kati ya vikundi 151 vilivyokopeshwa fedha hizo za asilimia 10 za mapato ya ndani kutoka kata zote 15 za Halmashauri ya Mji Tunduma.

"Uchunguzi umebaini kuwa kutorejeshwa  kwa mikopo hiyo ndani ya muda wa marejesho kumechangiwa na sababu mbalimbali, ikiwemo wakopaji kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya mikopo hiyo" amesema Wikesi.

Aidha,  Mkuu huyo wa Takukuru Mkoa wa Songwe amesema sababu nyingine zilizochangia  mikopo hiyo kutorejeshwa kwa wakati ni matumizi mabaya ya mikopo kwa kuwa baadhi yao hutumia fedha hizo kwenye matumizi binafsi nje na dhumuni la mkopo.

"Tumebaini pia baadhi ya wanavikundi kukimbia na fedha za mikopo hali ambayo  imesababisha baadhi ya wanavikundi wengine kuwalipia wenzao waliokimbia, mikopo kutolewa kwa makundi yasiyo na vigezo pamoja makundi yasiyo hai" amefafanua zaidi Wikesi.

Pia wamefuatilia   utekelezaji wa mradi ya maendeleo  39 yenye thamani ya shilingi milioni 13,412,222,945.09 katika sekta za Elimu, Maji, Afya, Kilimo na Miundombinu.

Amesema katika ufuatiliaji huo, miradi 16 yenye thamani ya shilingi milioni 8,249,687,597 ilibainika kuwa na mapungufu kiufundi ambapo tayari ushauri umetolewa ili wahusila waweze kufanya marekebisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI