NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Mwenge wa uhuru mwaka 2024 umeendelea na mbio zake katika Halmashauri ya Mbeya ambapo umetembelea na kukagua miradi mbalimbali na kuweka jiwe la msingi ikiwemo kituo cha afya Igoma na daraja la Imezu.
Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini Mhe. Oran Njeza na viongozi wengine mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi na Serikali wakiwemo mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbeya Mhe. Mwalingo Kisemba na mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbeya vijijini ni miongoni mwa viongozi walioambatana na viongozi wengine na wananchi kwenye kushuhudia miradi mbalimbali ikikaguliwe na mwenge wa uhuru.
Viongozi hao wakiwa katika kijiji cha Darajani kata ya Inyala kwenye mradi wa daraja la Imezu ambalo ijumaa hii (Agosti 30, 2024) limewekwa jiwe la msingi na mwenge wa uhuru 2024 viongozi hao wameeleza kuridhishwa na utekelezwaji wa mradi huo utakaoleta tija kwa wananchi wa Mbeya vijijini hasa kata ya Inyala.
Hii ni baada ya kujengwa na wakala wa barabara mjini na vijijini TARURA wilayani Mbeya kwa mamilion ya fedha.
"Ndugu kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa, kwakweli tunamshu
kuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa Mbeya vijijini Mheshimiwa Rais ametupendelea, nanialitarajia daraja kama hili kuja kujengwa huku kijijini! Ukija kwenye barabara tuko vizuri, hapa Inyala ametujengea barabara ya lami kutoka Inyala hadi Tembela,lakini kuna lami nyingine itajengwa kutuunganisha na wenzetu wa Malamba wilaya ya Mbarali, barabara ya Mbalizi Shigamba mkandarasi ameenda kukusanya vitendea kazi muda wowote atakuja kuanza kazi ya ujenzi kilomita 52 za lami pia barabara ya Mbalizi Chang'ombe Mkwajuni mpaka Makongolosi pia inajengwa kwa kiwango cha lami nayo mkandarasi anajiandaa muda wowote atakuja kuanza kazi kwahiyo Mbeya vijijini tunashukuru sana", amesema Mbunge wa Mbeya vijijini Mhe. Oran Manasse Njeza.
Kwa mujibu wa wananchi na viongozi wa kata ya Inyala, Daraja hilo (Imezu) mpaka sasa limeua watu watatu kutokana na ubovu wa mara kwa mara kabla halijajengwa kwa ubora hivyo kujengwa kwa daraja hilo kutasaidia kuokoa maisha ya wananchi wa kata hiyo.
Meneja wa Wakala wa barabara za mjini na vijijini TARURA wilaya ya Mbeya Mhandisi Boniface Kasambo amesema matarajio yao ni kumaliza mradi huo kufikia Oktoba mwaka huu.
"Muda wa utekelezaji wa mradi huu wa ujenzi wa Daraja la Imezu ni siku 240 na extension kwa maana ya muda wa nyongeza ni siku 144 kwa gharama ya Tsh.118,531,440 na tunatarajia kumaliza kumaliza ujenzi huu kabla hata ya muda ambao kimkataba ni Oktoba 2024", ameeleza Mhandisi Boniface Kasambo, meneja wa TARURA wilaya ya Mbeya.
Hata hivyo kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa Godfrey Mzava, ametembelea na kukagua daraja hilo na kuridhika na ujenzi akisema litakuwa mkombozi kwa wananchi kutokana na umuhimu wake kuunganisha vijijini mbalimbali ikiwemo Inyala na Darajani na Mwashoma pia kuwasaidia wananchi kusafirisha mazao yao.
Kauli mbiu ya mwenge wa uhuru mwaka huu ni "Tunza mazingira na shiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa ujenzi wa Taifa endelevu".
0 Comments